Urembo ni Kama Ua

Napasha kusisimua, wazi ikadhihirika,
Lipo jambo kutambua, wazoni ukaliweka,
Wapenda kujifutua, kujiona warembeka,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Nafahamu hujajua, mbele unavyojiweka
Ujana wakusumbua, utake kufahamika,
Huwezi kujiinua, kwa maringo kuinuka,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Kwengine wajiteua, kufanya unavyotaka,
Nasema kufafanua, utakavyo kusifika,
Taelewa ukikua, ubozi utakutoka,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Ni vema kujikwatua, vizuri ukapambika,
Jua ngozi huungua, ukabaki kuchomeka,
Lifikalo kubabua, hiyo sura takunjika,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Sasa wajifaragua, mweledi hujagutuka,
Wapenda kujiketua, ubaki kufahamika,
La wema hujaamua, kutwa utaaibika,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Urembo kama kilua, utapata kakauka,
Sasa unajiinua, kwenda chini ni dakika,
Huenda ukaugua, urembo ukachanika,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Heshima hutanunua, kwa mapeni kulipika,
Aibu ukichagua, itakuwa kuitaka,
Watu wamekubeua, kwa tabia wamechoka,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Hayo mambo umezua, watu hawajayataka,
Ulidhani kufumbua, usijue twaudhika,
Inabidi kutatua, vema hujabahatika,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Usaha nimetumbua, dhahiri limefichuka,
Tena nimechechemua, liweze kueleweka,
Vema ukaligundua, pale watu twakuweka,
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *