Maisha ni Kama Ua

Mwanadamu hajajua,  ukweli kueleweka,
Huringa kujifutua, asitabiri mashaka,
Ukweli hajang’amua, kutojua kumtoka,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

Maisha huwa murua, hatima huharibika,
Leo hili waamua, keshoye latatanika,
Ukweli hajatambua, vema ukatambulika,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

Vema hajagundua, vilivyo kuleweka,
Iwapo hajaungua, unguliko tamfika,
Kwa leo hujaugua, kesho mengi yachipuka,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

Ua jema huchanua, kwengi likatamanika,
Linang’aa bila jua,  kote likatambulika,
Jua likijipanua, ua linaharibika,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

Kifedha hujitanua, utajiri kupanuka,
Sana hujifaragua, kupenda kuinulika,
Maisha humpindua, kabaki alalamika,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *