Ulitunze Yai Langu

Yai langu la muhimu, lisipate haribika,
Hifadhi ulihishimu, pema ukaliweka,
Nifanyie ukarimu, mwisho nikafaidika,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la thamani, lisipate saujika,
Langalie kwa makini, nisije nikaudhika,
Litanipa purotini, siha nikanawirika,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la maana, vibaya lingavunjika,
Muda ukishawiana, lenyewe nitalitaka,
Moto utachukuana, kwa maji likachemka,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la mahaba, lisipate kudhurika,
Kutwa moja niwe baba, vema likiifadhika,
Mwisho usitowe toba, maasi yakikutoka,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la mawazo, lisiweze kutoboka,
Nimekupa maelezo, yaweze kufatilika,
Upate wangu mwongozo, taratibu kufanyika,
Ulitunzeyai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la baraka, hatima laangulika,
Vifaranga kufanyika, liwalo likatunzika,
Uvundo hautatoka, laana hitosikika,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la furaha, uliweke kufichika,
Hatima nipate raha, lifikapo la kulika,
Nisiikose buraha, shari nayo kunitoka,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

Yai langu la faraja, liweke kuhifadhika,
Ya muhimu nimetaja, yaho yatafakarika,
Nalitaka jambo moja, yai langu kutunzika,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *