Nimeshampata Mwali

Siti amenikubali, ombi nilipompasha,
Hakuola yangu mali, upendo ulimtosha,
Ana mema maadili, tabiaze zaridhisha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

Katu hakunikabili, ati kuniaibisha,
Hakufoka kwa ukali, pendo alinionesha,
Nami kampa ukweli, uongo sikumvisha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

Amependa yangu hali, penzi likamlewesha,
Tunaponena wawili, hana la kumnongesha,
Ameapa kunijali, kwema kuniabirisha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

Nitakuwa mhimili, hata iwe kumlisha,
Ameshanipa kibali, mbali nikamfikisha,
La talaka hajakuli, moyoni amenipisha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

Mambo yake ni kamili, hatendi likakutisha,
Napenda umbo la mwili, ila hatojionesha,
Sifa zake si kalili, daima humkumbusha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *