Unani Sogora?

Wadunda zinavuma, ufundi unao,
Hukosi adhama, fundi wa mwambao,
Ungetwanga ngoma, muda ufaao,
U nani sogora, kucha tusilale?

Piga nisilale, utakavyo tenda,
Hewani kelele, kwa wingi zatanda,
Hunalo la pole, jirani kupenda,
U nani sogora, kucha tusilale?

Nyingi raha zako, kwa wako muziki,
Twabaki kimako, tulivu hutaki,
Ndumo na mwomboko, wadai ni haki,
U nani sogora, kucha tusilale?

Ngoma hepasuki, udunde daima,
Yaileta dhiki, usiwe huruma,
Ewe hugutuki, woneshe hishima,
U nani sogora, kucha tusilale?

Lifanye la wema, mchana ucheze,
Kucha kalalama, sana ujilaze,
I papo lawama, hebu nikujuze,
U nani sogora, kucha tusilale?

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *