Chungu Nachomeka

Mafiga umeyapanga, mekoni kuniinjika,
Kuni umeshazipanga, kwa moto ukaniweka,
Nyinginezo wazichonga, moto wako kuukoka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Asubuhi uwe nami, staftahi kupika,
Kuniunguza hukomi, wadhani sitoudhika,
Una bahati sineni, nichomwe sitosikika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Chungucho sipumziki, upike nami kishuka,
Wadhani siunguliki, chakula chako nataka,
Wanigota sitamki, kwa mwiko unapopika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Hutoniacha jioni, chajio unakitaka,
Upike umenihini, chungu sitotambulika,
Ukigawa hunioni, kinakwisha cha kulika,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Usiku nimo motoni, wache supu kuchemka,
Kila wakati kazini, sina pa kupumzika,
Hunitii maanani, tamaa ikanitoka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Mpishi hunao wema, siati kunung’unika,
Hujaona nimegoma, kaziyo kutofanyika,
Wataka yangu huduma, ukipata watoweka,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Mfinyanzi alianza, motoni akaniweka,
Mpishi wa kunitunza, moto sijanusurika,
Kila wakati kukanza, mwenyewe hunufaika,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Vigae hutovitaka, mwenyewe nikivunjika,
Kila siku nateseka, wewe ukisaidika,
Motoni naungulika, ubaki wafurahika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Sizikosi haki zangu, hili likaeleweka,
Usije nitia pingu, mambo yako ukitaka,
Wadhani sina uchungu, motoni kuungulika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Asubuhi u nami, unitumie kishuka,
Jioni umejihami, kwako kazi kufanyika,
Kazi zangu hazikwami, chakula bado chalika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Masinzi tonge hayawi, bado sijaliwazika,
Kwangu katu hayaliwi, yakawa yanamegeka,
Nisemapo sisikiwi, majukumu wanitwika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Kujihami ni lazima, maneno nikatamka,
Nimeamua kugoma, chakula kutopikika,
Hamnalo la huruma, kwenye raha kuniweka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Hainitishi kejeli, hadi langu kusikika,
Nitabaki na la kweli, ili niwe natukuka,
Watazama yangu hali, udongo ukiucheka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

© Kimani wa Mbogo

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *