Jina Langu Libomoe

Naja nikwambie siri, iwapo hujui sana,
Shetani amekwajiri, uharibu langu jina,
Wadhani unayo heri, uendapo ukinena,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Mshahara mwingi sana, usubiri utapewa,
Mwishowe utauona, ujira kukabidhiwa,
Sikia ninalonena, sitaki kukashifiwa,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Kazi ulipoikosa, shetani alikwajiri,
Ukaseme langu kosa, ungojeapo dinari,
Wadhani unanitesa, wanitafutia heri,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Msemi nenda kaseme, utalipwa siku moja,
Uende ukalolome, hiyo ndiyo yako hoja,
Nenda mbele usimame, watangazie wateja,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Utaacha sitishiki, ukienda Jahanamu,
Mwenyewe sitikishiki, na ukweli utadumu,
Kusikia sikutaki, nitaipata elimu,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Utaiona aibu, shetani akikulipa,
Mwisho utakuwa bubu, utakapotapatapa,
Usidhani utatubu, lawama itanenepa,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

Ujira umewekewa, bosi wako akungoja,
Mshahara utapewa, kwa kazi niliyotaja,
Moto utaandaliwa, hiyo itakuwa hoja,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *