Aina za Mashairi

Mashairi huainishwa kwa kutumia idadi ya mishororo kwa kila ubeti. Zifuatazo ni aina za mashairi. Kwa mifano, tumetumia mashairi ya Kimani wa Mbogo.

1. Tathmina/umoja

Ni shairi lenye mshororo mmoja kwa kila ubeti. Mashairi haya ni adimu sana.

2. Tathnia

Ni shairi lenye mishororo miwili kwa kila ubeti. Tazama mfano ufuatao wa Miti Tuipande.

Tupande mbuni, iwe kahawa kinywani,
Kwa mdalasini, kiwe, kiungo mloni.

Mkaajabali, iwe dawa ya machoni,
Kwa mshelisheli, liwe tunda chemsheni.

Tupande mkanya, iwe dawa mauani,
Na kwa mvungunya,  mandhari mitini.

3. Tathlitha

Ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti. Tazama mfano wa shairi hili kuhusu Ushairi.

Shairi hung’aa, kwa ustadi utungapo,
Jema kuandaa, ushairi mwema upo,
Watu huduwaa, jema uliandikapo.

Haki itetee, usalama uwe kwako,
Tamu liwekee, japo vina vema viko,
Sifa zingojee, kwa umaarufu wako.

Waja elimisha, kupitia kwa shairi,
Bila kuwatisha, waelimishe ni heri,
Koja kukuvisha, halitakuwa la siri.

4. Tarbia

Ni shairi lenye mishororo minne kwa kila ubeti. Mashairi mengi ya Kiswahili huwa ya aina hii. Tazama mfano wa shairi hili Utokako Ukuole.

Yawaze yalokingama, uyasanifishe tele,
Usikose fanya wema, hisani uwafanyile,
Ijapofika kiyama, usiwe na la matule,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Likopanda vingulima, kosa usilirudile,
Chiniyo ukatazama. wendapo fika kilele,
Ulikopita dhalama, ola usiwe mtule,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Yarekebishe ya zama, usirudie yajile,
Usiyatende mafama, maovu kuliko mbele,
Baraka hukuandama, uwapo mwema mpole,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

5. Takhmisa

Ni shairi lenye mishororo mitano kwa kila ubeti. Tazama mfano ufuatao wa Tunda Tamu.

Lililo utamu, pachipachi likuapo,
Linipalo hamu, kila kutwa nililapo,
Linipalo jemu, mi nilitengenezapo,
Langu la muhimu, hilo ladha nipatapo,
Langu tunda tamu, hilo nilitafunapo.

Hilo lilo sumu, mara nyingi upatapo,
Lililo hukumu, ubichi ulitundapo,
Hilo silaumu, popote nilionapo,
Ni tunda adhimu, pale pote likuapo,
Langu tunda tamu, hilo nilitafunapo.

6. Tasdisa

Ni shairi lenye mishororo sita kwa kila ubeti.

7. Usaba

Ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti.

8. Ukumi

Ni shairi lenye mishororo kumi kwa kila ubeti.