Bahari za Ushairi

1. Ukara

Ukara ni shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine hubadilika. Kwa mfano, vina vya kipande cha mwisho vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho lakini vina vya kati vinabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.

Neno ukara asili yake ni ‘kara’ (wingi-makara) lenye maana ya kibanzi, kichane au kipande mithili ya kibandu cha gogo. Makara yakichanjwa kutoka kwa gogo lililosalia hufanana kwa upande mmoja tu na pande nyingine huwa na sura tofauti tofauti.

Katika mfano ufuatao, mtunzi ametumia vina tofauti upande wa ukwapi (-ko, -na, -wa) ila upande wa utao vina havibadiliki (-ni).

Mfano: Urembo Wako si Chochote

Kipusa una vituko, twaviola hadharani,
Vyanambukiza udhiko, nikaliweka tungoni,
Vimekupumbaza vyako, wakuu wakulaani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

Kitwani zavurungana, si zetu si za kigeni,
Nywele zaangukiana, kisogo na utosini,
Ukadhani unafana, wende zako kinarani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

Wajihi wajipodowa, podari imo usoni,
Sana umejikwatuwa, ukijeleza rohoni,
Dhahiri hujang’amuwa, umaridadi hunani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

2. Ukaraguni

Ukaraguni ni shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho hubadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.  Neno guni lina maana ya dosari au ila.

Ukaraguni lina asili ya naneno mamili; ukara na guni. Ukara ni mtindo wa kuvunja keketo za ukwapi pekee na kutiririsha zile za utao. Guni au dosari ni kwamba hakuna urari wa mizani na mishororo ila hazikuvunjavunja keketo zote za ukwapi na pia za utao. Watunzi walioshindwa kutunga mashairi ya mtiririko walibadilisha vina vya ukwapi na utao kwa kila ubeti na hatimaye ukaraguni kuwa bahari ya ushairi.

Katika mfano ufuatao, kuna  vina tofauti kwa kila ubeti na kila upande wa ubeti. Hili linatambulisha shairi hilo kuwa ukaraguni.

Mfano: Niache Nende Salama

Mja wa mateso miye, sina hili sina lile,
Waziwazi niambiye, sinibeze maumbile,
Singoje muda wadiye, kheri niambiwe mbele,
Miye dua nipigiye, Mwenyezi Yehova Jile.

Kazi ndiyo nitapata, pahali penye hishima,
Ujira mwingi kupata, licha ya njema huduma,
Changu cha pesa kitita, haki nipatge mapema,
Endapo utanifuta, niache nende salama.

Beti tatu zimetosha, sina muda kupoteza,
Kalamu nimekomesha, sina ya kusisitiza,
Mwajiri hutganitisha, mabaya ukitangaza,
Nipe ya pesa bahasha, japo hakuna nyongeza.

3. Mtiririko

Mtiririko ni shairi ambalo vina vyake vya mwisho na vya kati havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.

Mfano:Pananpo Moto Hufuka

Dhahiri hudhihirika, lionekalo hubaki,
Mahaba ujapoyataka, ukweli hautengeki,
Ungajitwika faraka, wa papo na mafasiki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Fichwalo hugundulika, usiwe huambiliki,
Ongea kutambulika, nyamaza husaidiki,
Lije la Kutatulika, atakufaa rafiki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Moshi ndo hutambulika, moto hausitiriki,
Pitapo palipowaka, halikosekani baki,
Kovu haitotibika, kabisa haikutoki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

4. Utenzi au Utendi

Shairi lenye kipande kimoja katika kila mshororo.  Neno ‘utenzi’ linatoka na kitenzi ‘tenda’ Historia ya ushairi imeelezea wazi kuwa utenzi/utendi ni mashairi yaliyotungwa kwa lengo la kuyakariri na kuigiza ujumbe huo. Tendi hizo ziltungwa kwa madhumuni ya kusimuliwa au kuimbwa pamoja na kuonyesha matendo na ishara zinazoambatana na kiini cha uimbaji huo. Sana sana tenzi zilihusishwa na maudhui ya kidini na imani ya jamii. Hata hivyo, mabadiliko mengi yamekuwa na watunzi wametungia nyanja tofauti za maisha ya mwanadamu. Tenzi huwa na beti nyingi zinazoelezea kisa/sifa fulani.

Mfano: Lawaridi

Palikuwa na banati,
Huyo angaitwa siti,
Kitongojini Kahati,
Zama alipozaliwa…

5. Mathnawi

Mathnawi ni shairi la vipande viwili (ukwapi na utao) katika kila mshororo. Mashairi mengi ya Kiswahili yametungwa kwa kutumia mtindo huu. Kati ya vipande hivyo viwili mshairi huainisha aghalabu kwa kutumia alama ya ‘koma’. Mwisho wa kila upande kwa kila mshoro kuna vina.

Mfano: Umesahau Ulikotoka

Hujawa nazo fadhili, vema ukaaminika,
Mali yasiyo halali, kwa hayo kabadilika,
Umejawa ukatili, ilikwondoka shabuka,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

6. Ukawafi

Ukawafi ni shairi la vipande vitatu (ukwapi, utao na mwandamo) katika kila mshororo. Si mashairi mashairi mengi ya Kiswahili yametungwa kwa kutumia mtindo huu.

Mfano: Majonzi Daima
Ufuatao ni mfano wa ukawafi.

Naliona ua, lililochanua, kaburi latua,
Moyo laumbua, na kuniungua, napolisekua,
Linanizuzua, kwa kuwachukua, na kunitandua,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

7. Mavue

Mavue ni shairi la vipande vinne katika kila mshororo.

Mfano: Liwate Wende Zako

Sikujui, bora wende, kwenu rudi, ujifite,
Sitambui, usishinde, huna hodi, chako kite,
Sikwinui, nikupende, la ahadi, uliwate,
Hugundui, ulitende, yakubidi, tu upite.

8. Mkufu/Pindu

Mkufu/pindu ni shairi ambalo neno la mwisho au kifungu cha mwisho cha maneno katika ubeti mmoja, hutangulia katika ubeti unaofuatia. Asili ya neno ‘pindu’ ni ‘pinda’ kwa maana ya mwendo wa zigizagi, mwendo mithili ya nyoka. Mshairi hutunga shairi ambapo maneno ya utao hukamatana na ukwapi wa ubeti unaofuata.

Mfano: Raha

Raha yangu kuposana, sana nilipe mahari,
Ari hijakosekana, kana uitwe fakiri,
Kiri mwenyewe kijana, jana ulivyotabiri,
Tabiri tajivunia, nia yangu ni furaha!

9. Kikwamba

Kikwamba ni shairi ambalo neno moja au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa kutanguliza mishororo au ubeti katika shairi. Asili ya neno hili ni neno la Kiswahili ‘amba’ linalomaanisha kusema, kunena au kuzungumza. Madhumuni ya mtunzi kurudiarudia neno fulani ni kusisitiza ujumbe wake kwa kutumia neno hilo.

Katika mfano ufuatao, mtunzi amesisitiza kuwa hajaweza lolote kwa kuwa hana ujuzi wa kutosha kutunga mashairi ipasavyo.

Mfano: Sijaweza

Sijaweza weupeni, matoni ninacho kiza,
Sijaweza kiotani, mwenyewe kudunduiza,
Sijaweza ya mitini, naona mauzauza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

10. Msuko

Shairi ambalo kibwagizo/mshororo wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo mingineyo. Kama (6,6) (6,6) (6). Neno hili linatokana na neno ‘suka’ lenye maana ya hali kadri ya kuridhisha. Mshairi basi hufupisha kibwagizo chake .

Tazama ubeti ufuatao kutoka shairi la Msuko. Mtunzi amefupisha mshororo wa mwisho.

Mfano: Neno la Adabu

Jambo uombapo, tafadhali sema,
Lako liwe lipo, laonyesha wema,

Kitu uombapo, omba kwa heshima,
Neno la adabu!

11. Kikai

Kikai ni shairi lenye kipande kimoja kifupi (chenye mizani chache kuliko kingine) Mfano (6,8) Neno lenyewe latokana na neno ‘kai’ lenye maana ya kusalimu amri au kuangukia mtu miguuni kama njia ya kukubali kushindwa. Katika historia ya ushairi mizani (8,8) kilikuwa ndicho kilele cha mshairi aliyefika kiwango cha umahiri. Basi aliyeshindwa kutimiza hizo mizani, alisalimu amri na kutumia mizani zilizopungua (8,8).

Kwa mfano, mtunzi ametumia mizani (4,8) kwenye ubeti huu wa shairi lake “Umeniwacha Mwandani”.

Mfano: Umeniacha Mwandani

Umeunda, nyingi raha mtimani,
Limetanda, sikitiko la huzuni,
Hujadinda, muhibu kuniauni,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

12. Mandhuma

Mandhuma ni shairi ambalo kipande kimoja hutoa hoja, wazo ama swali, huku cha pili kikitoa jibu/suluhisho.

13. Malumbano

Malumbano ni mashairi mawili ambapo mshairi mmoja hutunga shairi akijibu au kupinga utunzi wa mshairi mwengine.

Katika mfano ufuatao, mtunzi ametunga shairi la kumjibu mshairi mwengine aliyedai washairi wa pwani ndio bora zaidi.

Mfano: Somo ana Walakini

Ana yake Alamini, kuonesha hadharani,
Mada ya swifa hifani, imekolea utani,
Yafaa akabaini, watu wa bara si duni,
Somo ana walakini, kuwatetea Wapwani!

Ana mengi ya kulumba, tena muda wa kuamba,
Bara anavyowachimba, hajajua wametamba,
Heri ende zake chemba, kuliko ya kujigamba,
Somo macho amefumba, Wapwani akiwaremba.

14. Ngonjera

Ngonjera ni hairi lenye wahusika wawili wanaojibizana. Kwa mfano; ubeti wa kwanza, mtoto, na wa pili, mzazi.

Mfano: Waadhi wa Mzazi

MWANA:

Babangu ninalo swali, kwa kweli lanisakama,
Jicho unalo fahali, sitakwambia tazama,
Swali langu la fasili, hatupati hali njema,
Nieleze nielezwe, mbona tukose baraka?

BABA:

Ili upate baraka, kwa wazazi fanya vyema,
Hali njema ukitaka, mwena uwe na heshima,
Wazazi, dada na kaka, kwao iwe taadhima,
Mwanangu tega sikio, na heshima iwe ada.

17. Sabilia

Sabilia ni shairi lisilokuwa na kibwagizo. Kituo (mshororo wa mwisho) hubadilika kutoka ubeti hadi ubeti. Kusabilia ni kumwacha mtu afanye apendavyo ama kumpa uhuru. Katika mashairi ya Sabilia, kila ubeti una uhuru wa kuwa na kiishio kinachojitegemea.

Mfano: Ajifanyavyo Mwamuzi

Vilivyo hujionesha, tungo zake atungavyo,
Yuyo huyo kapotosha, anavyohadhiri sivyo,
Minarani hujinyosha, kwa tabia zake ovyo,
Kumbe kadharauliwa, mwamuzi mwenye adhama.

Hutangaza hatujui, mwamuzi mjua yote,
Madaha hayapungui, wandikalo alifute,
Ameshakuwa adui, marafiki asipate,
Mpate mwamuzi mui, ukiweza umfate.

Mwamuzi hujua mengi. ajuavyo ni mjuvi,
Maneno yake kwa wingi, mara alete ugomvi,
Mwamuzi yeye hatungi, uamuzi ndo ugavi,
Kinywache nacho hafungi, kelele kama mlevi.

16. Sakarani

Sakarani ni shairi lenye bahari zaidi ya moja. Neno sakarani linamaanisha kutenda jambo bila kuwa na akili timamu. Washairi walipokuwa katika harakati za kushindana ni nani katunga bora kuliko mwengine, walifanya kama watu waliorukwa na akili kwa kiu ya ubingwa. Hilo lilisababisha kutunga shairi moja kwa kutumia bahari zote.