Uchambuzi wa Mashairi

Uchambuzi au uhakiki wa mashairi ni kuvunjavunja shairi katika sehemu zake na kuzichunguza kwa makini ili kueleza ujumbe, dhamira, maudhui na hali ya vipengee vya shairi. Anayefanya uchambuzi wa mashairi huwa na mengi ya kuzingatia. Kwa kifupi, tuyaangazie baadhi ya masuala hayo.

Anwani

 • Huu ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi moja. Anwani ni kidokezo muhimu cha kinachozungumziwa katika shairi.
 • Anwani huwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya kibwagizo.
 • Shairi hupewa anwani inayoafikiana na maudhui au dhamira kwa  sentensi fupi.

Muundo/Umbo la Ushairi.

 • Umbo la shairi hujulikana kwa jinsi shairi lenyewe lilivyoundwa.
 • Umbo la ushairi hujulikana kwa vina, idadi ya mizani, mishororo na vipande.
 • Shairi pia hujulikana bahari lake kwa kuangazia vina. Ni vina vitakavyolitambulisha kuwa Mtiririko, Ukara au Ukaraguni.
 • Ni vema pia kutambua kama shairi lina mshororo unaorudiwarudiwa kwa kila ubeti. Mshororo huo wa mwisho unaorudiwarudia kwa kila ubeti huitwa kibwagizo au kiitikio.
 • Iwapo hakuna mshororo unaorudiwarudiwa, basi mshororo huo wa mwisho kwa kila ubeti huitwa kiishio au kimalizio.
 • Bonyeza hapa usome zaidi.

Maudhui.

 • Huu ni ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani.
 • Maudhui hutumiwa kujenga dhamira ya shairi. Kwa mfano: malezi, siasa, usalama, unyanyasaji, ufisadi n.k.
 • Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi kutokana na kisa kilichomo katika shairi.

Dhamira/Shabaha.

 • Hii ni mada, lengo kuu, wazo kuu, kusudi, madhumuni au nia ya mtunzi aliyokuwa nayo anapolitunga shairi lake.
 • Mtunzi wa shairi anaweza kuwa na makusudi mbalilmbali. Mashairi huweza kuwa na dhamira za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni. Mifano ya baadhi ya dhamira zinazoonekana katika mashairi ni pamoja na uongozi bora, mapenzi, dini, ndoa, elimu, kazi na ukombozi.
 • Mshairi hutunga shairi lake kwa lengo la kuelimisha, kuonya, kutahadharisha, kuliwaza, kuburudisha, kuhamasisha jamii, kukuza sanaa na ukwasi wa lugha, kuelekeza, kupitisha ujumbe, kusifia mtu au kitu, kukejeli, kukemea.
 • Baada ya kusoma shairi, unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli ipi.
 • Dhamira hutokana na mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.

Mtindo wa lugha.

 • Mshairi hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
 • Baadhi ya mbinu kama Tanakali za Sauti, Istiara, Takriri, au Semi.
 • Bonyeza hapa husome zaidi.

Ujumbe

 • Ujumbe ni yale mambo ambayo mshairi angependa hadhira ijifunze ili kuweza kufanikisha misimamo iliyojengwa na msanii huyo.
 • Kwa mfano, kama shairi linahusu mapenzi ujumbe unaweza kuwa “mapenzi yanaua, mapenzi yanapofanywa shuleni huweza kuathiri ujifunzaji na ufundishaji, mapenzi huweza kuwa faraja katika kipindi cha matatizo” na kadhalika.

Falsafa

 • Falsafa ni imani ya mshairi. Kipengele hiki huhusisha vipengele vya ujumbe, maadili na msimamo wa mshairi ambao hutokana na dhamira za kazi hiyo.
 • Mara nyingi falsafa hujitokeza katika namna mshairi anavyotoa masuluhisho ya migogoro inayojitokeza au mahitimisho anayoyatoa juu ya masuala mbalimbali. Falsafa inaweza kuwa “pindi wema na ubaya vinapopambana wema hushinda, malipo ya ubaya ni aibu, tamaa mbele mauti nyuma, asiyesikia la mkuu huvunjika guu, maisha hayana maana yoyote (kufa leo au kesho vyote ni sawa tu)” na kadhalika.

Uhuru wa mshairi.

 • Mshairi ana uhuru wa kutumia lugha vyovyote vile ilmradi tu utunzi wake uzingatie kanuni za ushairi.
 • Baadhi ya hayo ni kusawazisha mizani katika mshororo, kubadilisha silabi za mwisho kwa maana ya kustawazisha urari wa vina, kuboronga sarufi au kutohoa maneno.
 • Bonyeza hapa usome zaidi kuhusu uhuru wa mshairi.

Fundisho

 • Fundisho ni mafunzo ambayo tunajifunza kupitia shairi husika. Fundisho huhusiana na falsafa na mtazamo wa jamii kwa ujumla jinsi inavyoyaona mambo.
 • Mara nyingi fundisho huwa ni juu ya mambo mema, hatutarajii mhakiki aseme mshairi anaifundisha jamii juu ya umuhimu wa wizi katika kipindi cha matatizo. Uvutaji bangi ni kitu kibaya na katika jamii hakuna namna ya kuuhalalisha. Hivyo, fundisho huweza kuwa, kwa mfano, mwandishi anaifunza jamii kwamba ni muhimu kutilia maanani ushauri wa wakuu kwani asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

Msimamo

 • Msimamo wa mshairi huitwa pia mtazamo wa mshairi.
 • Msimamo ni jinsi mshairi anavyoyachukulia mambo katika ulimwengu au jamii husika anayoisawiri.
 • Msimamo si lazima kila wakati ukubalike na wanajamii wote japokuwa mafundisho yanayotolewa katika ushairi yanaweza kukubaliwa na jamii yote.