Tamathali za Usemi

Zifuatazo ni baadhi ya tamadhali za usemi na mbinu nyinginezo hupatikana kwa ushairi:

1. Tashbiha au Mshabaha

Huku ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kuwa vina mshabaha au mfanano wa sifa fulani. Maneno yafuatayo ya ulinganishaji hutumiwa maneno kama; sawa na, mfano wa, ja, kama au mithili ya.

Mshairi analinganisha mawaidha na ngao kwa mfano wa kwanza kwa kuwa mawaidha anayoyatumia kwenye shairi lake litamkinga mtoto/kijana kwa maovu ya ulimwengu. Katika mfano wa pili analinganisha urembo na ua kwa maana kuwa urembo huo ni muda tu, kutwa moja huisha. Mfano wa mwisho, amelinganisha maisha na ua kwa kuwa mwanadamu maisha yake huishia kifoni.

Mfano wa Kwanza: Watoto ni Baraka

Watu wana njia nyingi, wanavyolea wanao,
Kunayo mawaidha mengi, yaliyopo kama ngao,
Nielezeni kwa wingi, tunahitaji mazao,
Nataka mnieleze, mtalea mwana vipi?

Mfano wa Pili: Urembo ni Kama Ua

Ni vema kujikwatua, vizuri ukapambika, 
Jua ngozi huungua, ukabaki kuchomeka, 
Lifikalo kubabua, hiyo sura takunjika, 
Urembo ni kama ua, hujajua hunyauka!

Mfano wa Tatu: Maisha ni Kama Ua

Maisha huwa murua, hatima huharibika,
Leo hili waamua, keshoye latatanika,
Ukweli hajatambua, vema ukatambulika,
Maisha ni kama ua, kutwa moja hunyauka.

 2. Sitiari

Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili bila kutumia maneno ya ulinganishaji kama ilivyo katika tashbiha (1 hapo juu). Neno sitiari linatokana na neno sitiri lenye maana ya kufunika; kuziba au kuficha. Hivyo sitiari ni tamathali ya usemi ya mlinganisho ambayo kwamba kitu kimoja kinalinganishwa na kingine kwa kukisema kuwa kitu hicho ni kingine.

Mtunzi anamlinganisha Omar Babu Marjan kama mti kwenye mfao ufuatao na kujilinganisha yeye na wenzake washairi kama mche. Kwa maana yake, anamaanisha Omar Babu Marjan kama gwiji kwenye uwanja wa utunzi na kumaanisha yeye na wenzake ni chipukizi kwenye uwanja wa ushairi. Shairi lenyewe linatoa ulinganisho wa moja kwa moja bila maneno yanayotumiwa kwenye mbinu ya tashbiha.

Mfano: Wengine Tungali Miche

Lasifika lako jina, iweje unajikana? 
Utunzi wako wafana, hakunaye wa kuguna, 
Wenyewe tumeshaona, takuwaje sifa huna? 
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

 3. Jazada

Hii ni mbinu ya kutumia mafumbo ambapo mtunzi hutoa maelezo ya kitu kuwakilisha kitu kingine. Kwa mfano, ua au ndege hutumika kumaanisha mpenzi. Tausi hutumika kurejelea mtu mwenye kiburi au maringo.

Katika mfano ufuatao, mtunzi anatumia neno yai kuwa mpenzi. Yai lisipowekwa vizuri huvunjika. Analinganisha mpenzi wake na yai kwa kumaanisha ahifadhiwe vyema asipate majeraha ama maovu yoyote maishani.

Mfano: Ulitunze Yai Langu

Yai langu la mahaba, lisipate kudhurika,
Kutwa moja niwe baba, vema likihifadhika,
Mwisho usitowe toba, maasi yakikutoka,
Ulitunze yai langu, lisivuje kuvunjika.

 4. Majazi

Majazi ni hali ya kumpa mhusika, mahali au kitu jina linalofanana na tabia zake au baadhi ya sifa zake. Kwa mfano, Busara ni mutu mwenye hekima, Buraha ni mahali pa kupata furaha, Ghulamu ni kijana mwanamume na Siti ni kijana mwanamke.

Katika mfano ufauatao, mtunzi anamwita mpenzi wake Siti. Siti sio jina lake halisi limetumiwa hapo tu kwa kutumia mbinu ya majazi.

Mfano: Nimeshampata Mwali

Siti amenikubali, ombi nilipompasha,
Hakuola yangu mali, upendo ulimtosha,
Ana mema maadili, tabiaze zaridhisha,
Nimeshampata mwali, pekee ananitosha!

 5. Takriri

Takriri ni marudio ya sauti fulani za konsonanti au vokali au maneno katika mstari wa shairi.

Ubeti ufuatao umenukuliwa kutoka kwa shairi linaloitwa “Onesha”. Mbinu ya takriri imetumiwa katika upande wa ukwapi.

Mfano: Onesha Onesha!

Mwalimu mwalimu, tenda ya mwalimu,
Nidhamu nidhamu, kitu cha muhimu,
Mwalimu mwalimu, vema uhudumu,
Onesha onesha, wako ualimu.

6. Tasifida

Tasifida ni mbinu ya kutumia maneno ya heshima na adabu kuepuka maneno ya aibu na matusi. Maneno ya heshima yanayokubalika ni kama mjamzito, makalio, maziwa, kendesha, nk.

Katika mfano ufuatao, mtunzi ametumia neno maziwa badala ya matiti kwa kutumia mbinu ya tasifida.

Mfano: Nitongoze kwa mpango

Wabisha wangu mlango, chumba changu wakijuwa,
Uwazi wako mgongo, wanionesha maziwa,
Kumbe unayo malengo, wanijia kusumbuwa,
Nitongoze kwa mpango, kila mwendo ni hatuwa!

7. Balagha

Balagha ni mbinu ya kuuliza swali lisilohitaji kujibiwa. Anayeuliza huwa na nia ya kuchochea msikilizaji ili afuate mkondo wake wa fikira.

Katika shairi “Unani sogora?”, mtunzi ametumia mbinu ya balagha. Amekasirishwa na sogora anayefanya kazi yake usiku na kuuwafanya watu wasilale. Anapouliza ‘U nani sogora?” hahitaji wala kutarajia jibu. Hili ni swali la balagha.

Mfano: Unani Sogora

Wadunda zinavuma, ufundi unao,
Hukosi adhama, fundi wa mwambao,
Ungetwanga ngoma, muda ufaao,
Unani ewe sogora, kucha tusilale? 

8. Tashihisi, Uhaishaji au Uhuishi

Hii ni mbinu ya kuvipa vitu visivyo na uhai sifa na tabia za ubinadamu za kusema au kutenda.

Katika mfano ufuatao, chungu cha kupikia kimepatiwa sifa za binadamu kuongea. Chungu hiki kinalalamika kuwa kinatumiwa kila wakati kupikia ila hakipatiwi chakula kinachopikwa.

Mfano: Chungu Nachomeka

Mafiga umeyapanga, mekoni kuniinjika,
Kuni umeshazipanga, kwa moto ukaniweka,
Nyinginezo wazichonga, moto wako kuukoka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

9. Chuku au Udamisi

Mbinu hii hutumiwa kutia chumvi maelezo ya kitu ili kutoa sifa zake zaidi. Baadhi ya maelezo huwa si ya kweli kwa kweli si lazima yatokee maishani.

Katika mfano ufuatao, mbinu ya chuku imetumiwa. Mtunzi ametia chumvi kwa kuelezea ati moyo wake unadunda na hauna hisani kwa kuachwa na mpenzi wake.

Mfano: Umeniacha Mwandani

Unadunda, moyo hauna hisani,
Ulikanda, mwili wangu kuubuni,
Langu tunda, kaanguliwa mtini,
Umekwenda, umeniacha mwandani?

10. Kinaya

Hii ni mbinu ya kutoa maelezo ya kitu au hali iliyo kinyume na matarajio.

Ubeti ufuatao umenukuliwa kutoka kwa shairi linalojulikana kama “Jina langu libomoe”. Tunavyojua ni kuwa Jehanamu kutakuwa tu na adhabu. Hata hivyo, kutumia hili shairi mtunzi anaonysha kuwa mtu anayemharibia jina atalipwa huko.

Mfano: Jina langu libomoe

Mshahara mwingi sana, usubiri utapewa,
Mwishowe utauona, ujira kukabidhiwa,
Sikia ninalonena, sitaki kukashifiwa,
Jina langu libomoe, Jehanamu utalipwa!