Uhuru wa Mshairi

Mshairi ana uhuru wa kutumia lugha vyovyote vile ilmradi tu utunzi wake uzingatie kanuni za ushairi. Baadhi ya hayo ni kusawazisha mizani katika mshororo, kubadilisha silabi za mwisho kwa maana ya kustawazisha urari wa vina, kuboronga sarufi au kutohoa maneno. Zifuatazo ni namna za uhuru mtunzi anaotumia. Kwa mifano ifuatayo, tumetumia mashairi ya Kimani wa Mbogo.

1. Tabdili

Ni uhuru wa mwandishi kubadilisha sauti na neno ili kufananisha vina. Kwa mfano mtunzi anaweza kutumia neno “upudhi” badala ya “upuzi”. Tazama ubeti ufuatao kutoka kwa shairi Ajifanyavyo mwamuzi.

Hujipamba cheo kadhi, kumbe hana yake kazi,
Amezidisha upudhi, kwa ubaya wa malezi,
Hujibadikia hadhi, ila hanao ujuzi,
Kwa matuko anaudhi, ajifanyavyo mwamuzi!

2. Inkisari

Asili ya neno hili ni “mukhtasari”. Inkisari ni uhuru wa kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo. Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “sendi” badala ya “siendi”. Tazama ubeti ufuatao kutoka kwa shairi Afande hongo sitowi.

Darahimu sendi kopa, ofisaa sipagawi,
Ufisadi nitahepa, hela haziniokowi,
Kwa lake Mola naapa, zangu fedha haziliwi,
Afande rushwa sitowi, ufisadinaogopa!

3. Mazida

Asili ya neno hili ni “zidi” au “ziada”. Mazida ni uhuru wa kuongeza silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo. Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “desituri” badala ya “desturi” au “enenda” badala ya “enda”. Tazama ubeti ufuatao kutoka kwa shairi Atakupenda ulivyo?

Hata Mola kakulinda, utawaza na kukonda,
Zurura kote enenda, simwoni kipofu kinda,
Macho yake amewanda, kuona unachotenda,
Atakupendaulivyo, asipende uli’navyo?

4. Kuboronga Sarufi

Huu ni uhuru mtunzi anaotumia kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au mdundo wa ushairi.  Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “changu chambo ninakupa” badala ya “ninakupa chambo chambo”.  Tazama mfano ufatao. Mtunzi amesema’ “Lasifika lako jina” badala ya “Jina lako linasifika”. Ubeti umenukuliwa kutoka kwa shairi Wengine Tungali Miche.

Lasifika lako jina, iweje unajikana,
Utunzi wako wafana, hakunaye wa kuguna,
Wenyewe tumeshaona, takuwaje sifa huna,
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

5. Utohozi

Hii ni mbinu ya kuswahilisha maneno kwa kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.  Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “maikrowevu” badala ya “microwave.” Katika mfano ufuatao kutoka kwa Ashiki Wakati Usiofaa, mtunzi ametumia neno “Palupiti” ambalo ni utohozi kutoka kwa neno la Kiingereza “Pulpit”.

Kasisi anasikika, neno katupakulia,
Palupiti azunguka, itikadi kututia,
Kasula kajipachika, Masihi kuhimidia,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.