Itumie lugha inayoeleweka kwa watu wote. Unapoinena yako, na mimi yangu, tutaelewanaje? Lugha isiwe chanzo na msingi wa kukuza ukabila. Lugha Yako Sielewi


Lugha Yako Sielewi

Ninaamba kusikiwa, kunyamaa siambiwi,
Nawajia kuumbuwa, lugha hazizingatiwi,
Mkabila nielewa, lugha yako siijuwi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Maasi sijajaliwa, magombano siyazuwi,
mafumbo huyafumbuwa, lugha yako sifumbuwi,
Ukabila umejawa, aswili sifatiliwi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Lugha nyingi nasemewa, hakunayo siambiwi,
Uhasama natendewa, hisani hezingatiwi,
Domole kulifunguwa, utulivu siachiwi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Yako sitoing’amuwa, unitusi sigunduwi,
Wajinga ndio huliwa, kosa kunena siliwi,
Kwa lugha nikivamiwa, masengenyo sitombowi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Vitatizi nanenewa, kukuli sikubaliwi,
Yabidi kimya nijawa, nisemapo sisikiwi,
Makombora natiliwa, lugha tata sizijuwi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Husemi la kusikiwa, hilo sifafanuliwi,
Sinacho chako kipawa, lugha zako sizijuwi,
Magumu wayadondowa, nijuwayo huyatowi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

Nimechoka kuambiwa, lugha zenu sing’amuwi,
Naomba kunyamaziwa, nijapokuwa kiziwi,
Kheri niwe nakimbiwa, nikabakia siliwi,
Vema ukifafanuwa, lugha yako sielewi!

© Kimani wa Mbogo (26/03/2010)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*