Utunzi wa Mashairi

Utangulizi

Ushairi ni sanaa inayotumia mipangilio maalum ya maneno tofauti na nyimbo au kazi nyingine yoyote ya fasihi. Anayetunga shairi lazima afuate kanuni mbalimbali ili kupasha ujumbe kwa njia ya mkato. Hivyo basi, ni muhimu kujiandaa vyema ili aweze kupasha ujumbe kwa maneno machache atakayoyatumia katika shairi lake.

Sababu ya kutunga

Mara nyingi, mtunzi huwa na hisia ambazo humsukuma ili atunge kazi yake. Hisia zinaungana na mawazo ambayo humsumbua akilini mpaka aliwasilishe wazo lake ili hadhira ifahamu kilichopo moyoni mwake. Msukumo huo humwezesha mshairi kutunga ili apashe ujumbe wake.  Mtunzi hutungia tukio alilokumbana nalo kwa kuona, kusikia, kuhisi au kushuhudia.

Hoja za Kuzingatia

Mtunzi lazima azingatie hoja kama zifuatazo kabla ya kutunga:

 (A) UTAFITI

Lazima mtunzi afanye uchunguzi kuhusu suala analolitungia shairi. Kwa mfano, kutunga shairi kuhusu mnyama fulani lazima ufahamu sifa zake na maelezo kuhusu huyo mnyama kwa kina. Utunzi utakosa ladha iwapo mtunzi ametunga shairi kuhusu jambo asilolijua vyema.

(B) MAUDHUI NA DHAMIRA YA SHAIRI

Maudhui ni ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani. Dhamira ni mada, lengo kuu, wazo kuu, kusudi, madhumuni au nia ya mtunzi aliyokuwa nayo anapolitunga shairi lake. Lazima mtunzi awe na maudhui yatakayojitokeza kwenye shairi lake. Vipengele vya maudhui ni pamoja na migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo na dhamira za mwandishi.

 (C) BAHARI YA SHAIRI

Ni lazima mtunzi aamue aina ya shairi atakalolitunga kulingana na mtindo, umbo, vina, idadi ya mizani na matumizi ya lugha. Iwapo ni shairi la mtiririko, lazima mtunzi achague vina atakavyovitumia kutoka mwanzo hadi mwisho wa shairi lake bila kuishiwa na maneno. Wanaojifunza kutunga, hutumia vina vinavyopatikana kwa urahisi. Mfano, ‘ni’ huwa kwa maneno mengi ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na nomino zinazoongeza silabi ‘ni’ ili kuunda jina la mahali. Vina kama ‘dhi’, vina maneno machache sana ambayo huenda mtunzi akajitahidi sana ili kulikamilisha shairi lake.