Utendi wa Mwanakupona

Kuhusu Utendi wa Mwanakupona

Mwana Kupona binti Mshamu alizaliwa kisiwani Pate. Alikuwa mshairi wa Kiswahili katika karne ya 19 na alitunga Utendi unaojulikana sana katika fasihi ya Kiswahili.
Si mengi yanayofahamika kuhusu maisha ya Mwana Kupona binti Mshamu ila inajulikana alikuwa mke wa mwisho wa Sheikh Mataka. Sheikh Mataka alikuwa kiongozi wa Siu karibu na Pate kaskazini mwa Lamu, nchini Kenya. Inaaminika kwamba ukoo wao ulikuwa tajiri na wenye hadhi ya juu sana.

Sheikh Mataka na Mwana Kupona walijaaliwa wana wawili, Mwana Heshima na nduguye mdogo wa kiume, Muhammad. Bwana Mataka aliugua na kufariki mwaka wa 1856. Miaka miwili baadaye, Mwana Kupona akatunga utendi wake kama wosia kwa binti yake Mwana Heshima aliyekuwa na umri wa miaka kumi na minne. Mwana Kupona alifariki mwaka wa 1865 kwa maradhi yaliyohusiana na mfuko wa uzazi.
Inaaminika kuwa Muhammad bin Shee Mataka Al-Famau alikuwa kiongozi was Siyu kama babake. Alikuwa mshairi aliyepinga utawala wa Seyyid Majid na kufungwa ngomeni, Fort Jesus hadi kifo chake.

Inabainika wazi kwamba Utendi wa Mwana Kupona ulitungwa mwaka wa 1858 (mwaka wa 1275 kalenda ya Kiislamu). Ni utendi wa beti 102 zenye mafunzo na ushauri kuhusu ndoa na kazi za mke za nyumbani.
Katika ubeti wa kwanza, Utendi wa Mwana Kupona unaanza kwa utangulizi unaoelezea kuwa umetungwa na mama kwa mwanawe kama waadhi. “Njoo binti yangu nikushauri. Sifai tuzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sikiliza ushauri wangu, huenda ukauzingatia.”

Negema wangu binti 
Mchachefu wa sanati 
Upulike wasiati 
Asa ukazingatia.

Katika ubeti wa pili inakuwa wazi kuwa mtunzi (Mwana Kupona) alikuwa akiugua kwa muda. “Nimeugua. Ni mwaka mmoja sasa tangu nilipougua. Sijapata muda wa kukushauri.”

Maradhi yamenishika 
Hata yametimu mwaka 
Sikupata kutamka 
Neno lema kukwambia.

Katika beti zinazofuata, mtunzi anamshauri bintiye kwa ujumbe na lugha inayofana. Baadhi ya mambo anayoelezewa ni kama uhusiano mwema kati yake na atakayekuwa mumewe. Anaeleza bintiye kwamba, akielewa ujumbe wa utendi huu, kamwe hatasumbuka maishani. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya mambo ambayo Mwana Heshima anashauriwa.

Mafunzo kwa Uhusiano wa Mungu na Watu

  1. Kuwa na imani ya kidini kama wajibu wako
  2. Kuwa na adabu kila unapoenda
  3. Kuwa sadiki. Kila uambiwalo ulisikie na kulitenda
  4. Usifanye mambo ya ubishi watu wakakuchukia
  5. Kuwaheshimu watu wote unaokutana nao
  6. Usifanye kiburi
  7. Anayekupenda mpende

Mafunzo kwa Uhusiano wake na Mumewe

  1. Keti naye kwa adabu, usimtie ghadhabu na akinena usimpinge
  2. Atakalo usimhini
  3. Akitoka umuage na akirejea umkaribishe na kumpa mahali pazuri pa kupumzika
  4. Akilala umpapase na uhakikishe hakosi upepo
  5. Usimnenee kwa mayowe
  6. Mpikie na kumwandalia maakuli ili mwili umtuze
  7. Umnyoe, sharafa umtengeze na udi umfukize kila siku
  8. Mtunze kama kijana mdogo
  9. Amri zake usikatae na Mungu atakulipia
  10. Valia mavazi mema na ujipambe
  11. Nyumba yako iwe nadhifu
  12. Msifu mume wako na sifa zake uzieneze
  13. Jua anayoyapenda na ufuate hayo
  14. Ukitaka kutoka muombe ruhusa, akikataa kaa nyumbani
  15. Fuata idhini yake na ukikaa usikae sana njiani
  16. Ukirejea kaa naye utengeze matandiko ya kulalia
  17. Usimshurutishe kutoa kile ambacho hawezi
  18. Anachokupa kipokee na ukifurahiye
  19. Tabasamu na akwambialo ulielewe

Kutoka ubeti wa 68 mtunzi ameliweka ombi lake kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumsaidia kwa maneno aliyotaja. Pia anawaombea watu wote. Zipo baadhi ya beti pia ambazo zimeelezea kuhusu maisha ya mtunzi na uhusiano kati yake na mumewe. “Baba yako alinioa kwa sherehe za kufana. Tuliheshimiana siku zote tulizoishi pamoja”

Alinioa babako 
Kwa furaha na kicheko 
Tusondoleane mbeko 
Siku zote twalokaa.

“Mauti yake yalipomkabili, alinibariki sana. Kwa shukran na amani alifariki na nikaridhika moyoni.”

Yalipokuya faradhi 
Kanikariria radhi 
Kashukuru kafawidhi 
Moyo wangu katoshea.

Katika ubeti wa 92 anaelezea sababu ya kutunga utendi wake. “Sababu ya kutunga si liwe tu shairi au tungo ya malenga bali ninataka kumuusia binti yangu Mwana Heshima”

Na sababu ya kutunga 
Si shairi si malenga 
Nina kijana muinga 
Napenda kumuusia

Mwishoni (ubeti 97-99) anaelezea kuhusu mtunzi na mwaka ambao utendi huo ulitungwa. “Mtunzi wa utenzi huu ni mjane mwenye huzuni. Mwenyezi Mungu atamsamehe dhambi zake kuu.”

Mwenye kutungo nudhumu 
Ni bharibu mwenye hamu 
Na ubora wa ithimu 
Rabbi tamghufiria.

“Jina la mtunzi wa utenzi huu ni Mwana Kupona Mshamu aliyezaliwa kisiwani Pate.”

Ina lake mufahamu 
Ni mtaraji karimu 
Mwana kupona mshamu 
Pate alikozaliwa.

“Utenzi huu ulitungwa mwaka wa 1275 kalenda ya Kiislamu (hii ni sawa na mwaka wa 1858)”

Tarikhiye kwa yakini 
Ni alifu wa miyateni 
Hamsa wa sabini 
Hizi zote hirijia.

Wasifu wa Mwana Kupona (Malenga Kutoka Lamu)

Prof. Kitula King’ei ameelezea mengi kuhusu Utendi wa Mwana Kupona katika kitabu chake Wasifu wa Mwana Kupona (Malenga kutoka Lamu). Kitabu hiki kilitolewa na Longhorn Publishers Ltd mwaka wa 2008. Hili ni toleo la Kiswahili kando ya toleo la Kingereza linalojulikana kama Mwana Kupona: Poetess From Lamu.
Katika kitabu hiki kuna hadithi ya kufana inayosimulia kuhusu Mwanakupona, aliyekuwa malenga kutoka Lamu na mtunzi wa Utendi huo unaotajika.

Mwanakupona alikuwa akiugua kwa muda mrefu baada ya mumewe Shee Mataka kufariki. Bintiye Mwana Hashima alikuwa na umri wa miaka 16 na alikuwa na nduguye mdogo wa kiume. Katika novela hii, Kitula anasimulia kuhusu harusu ya kufana ya rafiki yake Mwana Hashima aliyeitwa Zuhura.

Mwanakupona anajihusisha katika utunzi wa Utendi uliokuwa kama wosia kwa bintiye Mwana Hashima. Ni utendi uliokuwa wa kumpa mwongozo katika maisha. Utendi huo wenye kutajika unaelezewa kuwa ulitungwa kwa kutumia lugha yenye taswira na sitiari anuwai.
“Utenzi ninaoukutungia hauna taswira na jazanda nyingi kwa sababu nilitaka uwe wenye kueleweka kwa urahisi. Sikutaka kutatiza msomaji kwa kumfanya kutafakari sana kuhusu maana za maneno au mafumbo.” Mwanakupona akielezea bintiye Mwana Hashima kuhusu utenzi wake. (Wasifu wa Mwana Kupona, Kitula King’ei uk. 52)

“Maneno yaliyomo katika beti za utendi huu yatasimama badala yangu na kuwa mkufunziwao pale nitakapohama duniani.”

Kitabu hiki pia kimeelezea kuwa Mwanakupona aliishi kwa maisha ya utajiri. Familia yake ikionekana kuishi mtaa wa kifahari na wakihudumiwa na Kitwana na Mjakazi.

“Ile nyumba iliukabili Msikiti wa Pwani kwa upande wa Kaskazini. Sehemu hiyo ya Kaskazini ndiyo iliyokuwa na majengi ya kuvutia sana na yenye hadhi katika nji mzima wa Lamu.” (uk 3)

Mwana Hashima ameelezewa kuwa mtu aliyeuliza maswali sana kwa hamu ya kutaka kujua. Mara nyingi anaoneka akimuuliza mama yake maswali, mengine yakiwa ni ya kukera.

“Hashima! Mwanangu! Swali la aina gani!” Mwanakupona alimuuliza bintiye (uk 32)

“Mzee Abubakar alifahamu udadisi wa msichana huyu naye Hashima alipendelea kujibiwa maswali na Mzee Abu, kama walivuozoea kumwita.” (uk 69)

“Mwana hashima ana kiu ya kipekee ya kudadisi mambo na kuuliza maswali yanayomsumbua mwenye kuulizwa.” Mwana Kupona akimwelezea Fatuma kisiwani Pate. (uk 83)

Wakati mwingi Mwanakupona alikuwa akitunga na wakati mwingine akimfunza binti yake kuhusu utunzi wa Utendi.

“Utendi ni shairi refu sana lenye beti nyingi ambalo aghalabu huwa na maudhui ya kihistoria, dini au kuhusu maisha ya mashujaa katika jamii. Huu ndio ushairi uliopendwa sana na watunzi wengi maarufu katika jamii ya Waswahili wa mwambao wa Afrika Mashariki… Utendi ndio utanzu wa ushairi ulio na lugha ya kikale lakini pia unaweza kitungwa kwa maneno au usemi wa kisasa. Lugha yake ni yenye mvuto mkubwa na mistari yake huwa mifupi. Ukiweza kutunga beti za utendi bila vikwazo vingi, basi unaweza kutunga aina zingine za ushairi kwa urahisi.” (uk 54)
“Mishororo mingi (ya utendi) huwa na mizani nane na kila ubeti huwa na mishororo minne yenye vina vya mwisho pekee vinavyofanana katika mistari mitatu ya kwanza na huku msitari wa nne ukiwa na kina maalum cha kituo chenye kufanana katika utendi mzima.” (uk 55)

Baadaye Mwanakupona, Mwana Hashima na kijana Mohammed wanafunga safari kuelekea kwa Fatuma aliyeishi kisiwani Pate. Mwanakupona alitaka kumwachia huyo rafiki yake dhamana kubwa ya kumtunzia mwanawe atakapokuwa amehitari dunia.

Aidha, ni kitabu ambacho kimeelezea mengi kuhusu ushairi wa kiswahili hasa utunzi.

“Ushairi ni zaidi ya kupanga mizani, vina na taswira au mafumbo. Shairi hutungwa kwa madhumuni fulani ya kijamii wala sio kwa ajili ya kulinganisha fu mizani au vina.” (uk 63)

Kwa ufupi, Utenzi wa Mwana Kupona ni mojawapo ya tenzi ambazo ni kama nguzo za ushairi na maisha kwa jumla. Ni utenzi unaoelezea na kuusia hisia tofauti katika maisha ya ndoa, uhusiano mwema katika jamii na kumcha Mwenyezi Mungu. Ingawa dunia imebadilika tangu utenzi huo kutungwa, waadhi uliopo huenda ukafaa kizazi kilichopo na vijavyo. Utunzi huo pia unaweza kuhifadhiwa kama kumbukumbu ya historia ya ushairi wa Kiswahili.