Uainishaji Kuzingatia Muundo

1. Sabilia

Sabilia ni shairi lisilokuwa na kibwagizo. Kituo (mshororo wa mwisho) hubadilika kutoka beti mmoja hadi mwingine. Kusabilia ni kumwacha mtu afanye apendavyo ama kumpa uhuru. Katika mashairi ya Sabilia, kila ubeti una uhuru wa huwa na kiishio kinachojitegemea.

Mfano:

Hutonipata makazi, nyumbani napumzika, 
Japo ninao ujuzi, mapeni yametoweka,
Mifuko ina uwazi, sina pa kufurahika,
Ninavyoifanza kazi, ninazidi kuteseka.

Nimebaki nikiwaza, kila kutwa nateseka,
Kujimudu sijaweza, hifadhi nikaiweka,
Mbele yangu kuna kiza, sijui nitavyovuka,
Kila ninapojikaza, moyo wangu navunjika.

Sifaulu kwa bidii, kwa lolote nalotaka,
Napojaribu kutii, mwasema nimepotoka,
Ubongoni situlii, imebidi kugutuka,
Jasho silifurahii, ya sulubu nayofanyika.

(Kimani wa Mbogo)

Katika shairi hili, mshairi ametumia kituo tofauti kwa kila ubeti.
Ubeti wa Kwanza: Ninavyoifanza kazi, ninazidi kuteseka.
Ubeti wa Pili: Kila ninapojikaza, moyo wangu navunjika.
Ubeti wa Tatu: Jasho silifurahii, ya sulubu nayofanyika.

2. Sakarani

Maana ya neno ‘Sakarani’ ni kuchanganyikiwa. Katika historia ya ushairi, washairi waliwania kuvikwa taji ya ubingwa kulingana na kazi zao. Jambo hilo lilichangia washairi kuchanganya bahari nyingi katika shairi moja.

Mfano:

Tenda mema,
Ya huruma,
Taadhima,
Ni maadili.
Usiwanie kuvuma,
Tenda kwa wako mtima,
Si utumwa ya heshima,
Ukarimu ni muhimu.

Umpataye njiani, heri umpishe vema,
Mtendee la hisani, bila jambo la hujuma,
Muhimu wako uneni, lolote unalosema.

Tenda mema uridhishe, utendalo la huduma,
Unaponena upashe, yakutoke ya hekima,
Ukarimu uoneshe, fadhila kukuandama,
Litende la maadili, ni muhimu kwa jamii.

 (Kimani wa Mbogo)

Katika mfano huu mtunzi ametumia bahari nyingi kwa shairi moja. Beti za kwanza mbili zina mtindo wa Utenzi, ubeti wa tatu ni Tathlitha na wa nne ni Tarbia.

3. Kikwamba

Kikwamba ni shairi ambalo neno moja au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa kutanguliza mishororo au ubeti katika shairi. Asili ya neno hili ni neno la Kiswahili ‘amba’ linalomaanisha kusema, kunena au kuzungumza. Madhumuni ya mtunzi kurudiarudia neno fulani ni kusisitiza ujumbe wake kwa kutumia neno hilo. Kuna mikondo mingi ya kikwamba kutegemea mahali au namna ya neno lililorudiwa.
Mtunzi wa shairi la kikwamba anaweza kurudiarudia neno la kwanza katika kila mshororo. Tazama mfano ufuatao.

Mfano 1:

Mpende uaminiye, moyo uwe kwa amani,
Mpende akutunzaye, akuenzi maishani,
Mpende akuenziye, atakuweka moyoni,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende akujuaye, kwa furaha na huzuni,
Mpende akupaye, muda wake maishani,
Mpende uliyenaye, humjui wa pembeni
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende umpendaye, ufurahiye moyoni,
Mpende ufurahiye, papatiko utoweni,
Mpende akupaye, tabasamu maishani,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende umpataye, siangalie watani,
Mpende usipaguye, rangi wala kabilani,
Mpende a’toleaye, kwa dhati toka moyoni,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende akubaliye, kuwa nawe maishani,
Mpende akubaliye, hali yako maishani,
Mpende akujuaye, huna hela mfukoni,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende asikizaye, sikioni na moyoni
Mpende asikizaye, unenapo kimiani,
Mpende aelewaye, tabasamu na huzuni,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

Mpende uchaguaye, uridhike mtimani,
Mpende u’tazamaye, na kumtia machoni,
Mpende ‘karibiaye, na mvuto u moyoni,
Mpende akupendaye, ataijua thamani.

(Justine Bin Orenge)

Mtunzi wa shairi la kikwamba anaweza kurudiarudia neno la kwanza katika kila kipande cha mshororo. Tazama mfano ufuatao.

Mfano 2:

Kiswahili kihimizwe, ni lugha ya kiungwana,
Kiswahili kipendezwe, ni lugha ya kufunzana,
Kiswahili silegezwe, ni lugha ya kukazana,
Kiswahili na kifunzwe, lugha ya kuongoana,
Kiswahili kitukuzwe, ni lugha ya kuambana,
Kiswahili kisikizwe, ni lugha ya kupangana,
Kiswahili kiongozwe, ni lugha ya kufaana,
Kiswahili na kifunzwe, lugha ya kuongoana.

Kiswahili na kikazwe, ni lugha ya kupendana,
Kiswahili sikatazwe, ni lugha ya kwelewana
Kiswahili na kifunzwe, lugha ya kuongoana.

Kiswahili sipuuzwe, lugha ya kutangamana,
Kiswahili kisibezwe, lugha ya kusemahana,
Kiswahili kisisazwe, ni lugha ya kushindana,
Kiswahili na kifunzwe, lugha ya kuongoana.

(Mwangi wa Githinji)

Katika mkondo mwingine wa kikwamba, mshairi anaweza kurudiarudia neno la kwanza la mshororo wa kwanza kwa kila ubeti. Tazama neno Nguruwe katika mfano ufuatao.

Mfano 3:

Nguruwe ninavyoamba, nasaili mnijibu,
Kwa mafumbo sitafumba, nasema wazi ajabu,
Wema hamjanipamba, jina langu mwaharibu,
Unono nilio nao, kwa huo mwanidharau?

Nguruwe sina bahati, watu mnanilaani,
La utulivu sipati, nifurahie amani,
Palipo watu sipiti, kwangu msiwe makini,
Ninavyovila vichafu, kwa hivyo mwanipuuza?

Nguruwe sina la vita, kila kutwa hutulia,
Sifa njema sijapata, kwa mema kuniswifia,
Mwanihujumu kutweta, ili nikaangamia,
Pepo nilizotupiwa, kwa hizo mwanilaani?

(Kimani wa Mbogo)

Iwapo shairi halina kibwagizo, basi maneno ya kituo yanaweza kurudiwarudiwa ili kusisitiza ujumbe fulani. Katika mfano ufuatao. Kifungu Mwajiri una kimerudiwa katika kila mshororo wa mwisho wa ubeti.

Mfano 4:

Nimetenda ya huduma, japo machungu nameza,
Ya suluhu nasukuma, malipo hujaongeza,
Nakupachika lawama, sinalo la kunyamaza,
Mwajiri una dhuluma, unatenda ya kubeza.

Unawania kuvuma, kishujaa watokeza,
Kwa anasa umezama, kwingine yanapooza,
Kutoa inakuuma, bilioni wawekeza,
Mwajiri una hujuma, unatenda kuchukiza.

Mimi sina kwangu kwema, kila kitu nimeuza,
Yangu yote yamekwama, umefifia mwangaza,
Ninasubiri Karima, aondoe kiambaza,
Mwajiri una hatima, unatenda kufukuza.

(Kimani wa Mbogo)

Maneno yanayorudiwarudiwa huenda yakawa hata mwisho wa mshororo au kipande. Tazama mfano ufuatao.

Mfano 5:

Nenda ofisini, hawajali,
Nyingi tafashani, hawajali,
Dhamana huhini, hawajali,
Kwa nini? Kwa nini?

(S. A. Mohamed, Longman Kenya,  Sikate Tamaa, Uk. 18)

Mfano 6:

Mkono wa mkulima, ni mgumu kama chuma,
Chakula cha mkulima, ni maharagwe na sima,
Mtazame mkulima, hapendezi hana dhima,
Bali huyu mkulima, ndiye chanzo cha uzima.

(Wallah Bin Wallah E.A.E.P, Malenga wa Ziwa Kuu, Uk 119)

4. Pindu/Nyoka/Mkufu

Pindu ni aina ya shairi ambapo neno la mwisho la mshororo wa mwisho wa ubeti linatumiwa kama kianzio cha ubeti unaofuata. Wakati mwingine neno la mwisho la ukwapi hurudiwa kuanza kipande cha utao.

Mtunzi anaweza kurudia neno au kifungu cha mshororo wa mwisho wa ubeti kutanguliza ubeti unaofuata. Tazama mfano ufuatao.

Mfano:

Ewe la-azizi, uloniepuka,
Kama mkimbizi, anavyotoroka,
Regea mpenzi, bado nakutaka.

Bado nakutaka, yako mazowea,
Nilivyokuweka, hakutegemea,
Nilinawirika, kwa njema afia.

Kwa njema afia, nimeneemeka,
Nikategemea, kwa kunenepeka,
Umenikimbia, naona mashaka.

(M. Kamal Khan, Tujifunze Mashairi, Macmillan Press, Uk 54)

Wakati mwingine mizani mbili za mwisho katika kipande cha mshororo hutumika kama neno la kutanguliza kipande au mshororo ufuatao.

Kukupasha sitasita, sita kwa vyangu vitendo,
Tendo utakalopata, pata kwa wangu mtindo,
Tindo inavyovikata, kata na wangu mkondo,
Kondo kwangu hutapata, pata nakupa upendo.

Pendo lisilo jeraha, raha itaeleweka,
Weka mbele kama tufaha, fahamu kabusurika,
Rika lisilo madaha, dahari lahishimika,
Mikasa hitowapata, pata nakupa upendo.

Pendo ni kuvumilia, liamini nalotaja,
Taja la kukutakia, kiapo unapongoja,
Ngoja kukuahidia, dia kwangu hitakuja,
Kujali utakupata, pata nakupa upendo.

(Kimani wa Mbogo)