Tumaini la kila mzazi kwa mtoto ni kwamba atafaulu hatimaye. Hivyo basi, mzazi huwa na jukumu kubwa kumshauri mwanawe. Humrekebisha na kumwongoza kwa njia inayofaa bila kuchoka. Waadhi na Wasia wa kila mzazi! Nakupa Wangu Wasia


Nakupa Wangu Wasia

Uyaole ya dunia, hangaiko yasikupe,
Kwayo mazuri tulia, usije kuwa mapepe,
Uwe mwema kwa tabia, daima moyo ujipe,
Nakupa wangu wasia!

Mwanangu usijipende, kwa mwenendo uwe mwema,
Maisha ukayashinde, kwa hishima na huruma,
Kwa raha usijiponde, zikakuweza tuhuma,
Nakupa wangu wasia!

Enenda shule kusoma, elimu ikuongoze,
Jizolee kubwa dhima, kutenda mengi uweze,
Usiwate taadhima, kila kutwa itukuze,
Nakupa wangu wasia!

Furahi ufurahie, kwa hekima ujipambe,
Waja wakutamanie, unavyokosa uzembe,
Pa ibada uingie, mfinyanzi akuumbe,
Nakupa wangu wasia!

Utafute mke mwema, uoe na kumpenda,
Ikuongoze neema, malezi bila kudinda,
Maovu ukiyatema, mema nayo kuyatenda,
Nakupa wangu wasia!

Maoni 8 ya “Nakupa Wangu Wasia”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*