Uainishaji Kuzingatia Mizani

1. Msuko

Hili ni aina la shairi ambapo mshororo wa mwisho kwa kila ubeti (Kibwagizo) umefupishwa makusudi. Yaani una mizani michache kuliko mishororo iliyotangulia.

Mfano:

Ni mwaka wa uchaguzi, chagua umpendae,
Uchague kwa ujuzi, na fujo uikatae,
Na ni wengi wagombezi, hongo pia ikatae,
Chagua umpendae.

Kampeni tangu majuzi, zinafanyika mchana,
Kuzunguka kuwa kazi, na ngoma kupigwa sana,
Wafuasi na wagombezi, mikono washashikana,
Chagua umpendae.

Tena kumbe siku hizi, vijana ni wengi sana,
Wanapokula mandizi, wanarukaruka sana,
Kutwa nzima kwao kazi, imepamba moto sana,
Chagua umpendae.

Vileo vyawekwa wazi, unaviona mchana,
Kuku na nyama za mbuzi, kwingi zimeliwa sana,
Pesa zatolewa wazi, vikundi vinagawana,
Chagua umpendae.

Pewa pesa kula mbuzi, imba na kuruka sana,
Halafu ukibalizi, fikiria tena sana,
Kura yako sio ndizi, ujue ina maana,
Chagua umpendae.

Mimi na wewe ni wazi, tuchague vyema sana,
Tuchague viongozi, walio na sifa sana,
Sifa nzuri na za wazi, walio na utu sana,
Chagua umpendae.

(Joel mburia “Rangile”)

Huu ni mfano kutoka kwa shairi la msuko. Mishororo ya kwanza mitatu kwa kila ubeti ina mizani 16 kwa kila mshororo lakini kibwagizo kimefupishwa. “Chagua umpendae.” ni mshororo wenye mizani 8.

2. Tenzi/Tendi

Utenzi ni shairi ambalo huwa na kipande kimoja cha mishororo. Huwa na mizani michache katika kila mshororo aghalabu baina ya nne na kumi na mbili (4-12). Huwa na kina kimoja tu kwa kila mshororo na beti nyingi. Tenzi zilitungwa ili kusimuliwa, kuimbwa au kuigizwa. Utenzi husimulia kwa mapana ma marefu maudhui ya kihistoria, kisiasa, kinyumbani, waadhi, mtu mashuhuri katika jamii miongoni mwa mambo mengine. Kila mshororo humalizika kwa kina kisichobadilika katika mishororo mitatu ya kwanza.

Vina hivi huitwa vina-vituo kwa jinsi vinavyolingana. Kina cha mshororo wa nne, ni tofauti lakini kwa kawaida hulingana na vingine vya kila mshororo wa nne wa kila ubeti. Vina hivi huitwa vina-vipokeo au bahari. Madhumuni ya kina kipokeo kutobadilika kutoka ubeti hadi ubeti ni kuufanya utenzi uwiane kwa beti zote.

Mfano wa bahari hii ni Utenzi wa Mwana Kupona uliotungwa mwaka wa 1858. Katika utenzi huo wa beti 99, Mwana Kupona anamshauri bintiye kuhusu ndoa na kazi za mke nyumbani. Mifano mingine ya tenzi ni kama Utenzi wa Fumo Liyongo, Utenzi wa Al-Inkishafi na Utenzi wa Ayubu.

Tazama mfano wa beti zifuatazo zilizonukuliwa kutoka wa utenzi.

Mfano:

Nilikuwa nikiwaza,
Sina wa kuniongoza,
Shida zikajitokeza,
Hukuja kunithamini.
Ukata ulitawala,
Tulikwazwa nazo mila,
Kati yao wenye hila
Nilizawa Mawazoni.
Kiatu ni ukubwani,
Ukata ulituhini,
Chozi likawa machoni,
Nani aletulaani?
Wazazi walijikaza,
Vitu vingi waliuza,
Toto hawakudekeza,
Yalo mengi kutuhini.
Mararu yalitufaa,
Machache tuliyovaa,
Kwa afya tulisinyaa,
Hatukupata sabuni.

(Kimani wa Mbogo)

Kina cha mwisho –ni kimerudiwa katika kila mshororo wa mwisho wa kila ubeti. Kina hiki ndicho kinachoitwa bahari. 

3. Gungu

Gungu ni shairi lenye mishororo mirefu aghalabu zaidi ya 12. Mashairi ya aina hii huwa na kipande kimoja tu cha mshororo na kina kimoja kwa kila mshororo. Yalitumiwa kama nyimbo za Waswahili. Tofauti na Utenzi, gungu huwa na mishororo mirefu iliyo na mizani zaidi ya 12. Mfano wa gungu ni “Mawaidha ya Wamuchuthe”.

4. Kisarambe

Kisarambe ni shairi ambalo huwa na mizani kumi na moja kwa kila mshororo na huwa na bahari kama utenzi. Kipande cha kwanza cha kila mshororo (ukwapi) hutoa swali au hoja ambayo hujibiwa katika kipande cha pili cha mshororo (utao). Aina hii ya mashairi pia huitwa mandhuma.

Mfano:

Tata zikishinda, hazitatuki,
Unalolitenda, halitendeki,
Jambo likivunda, haliongoki,
Tata zikiganda, haziganduki,
Utakapokwenda , zitakudhiki,
Moyo utadunda, kutaharuki,
Tata hukuzinda, ukahiliki,
Zikakupa inda, ukahamaki,
Unaloliwinda, halipatiki.

(Hassan M. Mbega, Longman Kenya)

5. Shairi Guni

Shairi-guni ni utunzi unaoonekana kama shairi halisi lakini kwa hali fulani ukashindwa kufuata na kukamilisha arudhi za ushairi. Shairi-guni ni shairi halisi kwa umbo, lakini lililo na ila.

Tazama ubeti ufuatao unaooneka kuwa wa Tarbia.

Mja wa mateso miye, sina hili sina lile,
Dhahiri niambiye, usinibeze maumbile,
Usingoje muda uwadiye, kheri unijuze mbele,
Waja dua nipigiye, nipate baraka tele.

(Kimani wa Mbogo)

Japo utungo huu unaonekana kuwa ni ubeti wa shairi, haujatimiza arudhi zote ta ushairi. Huu ni mfano wa ubeti kutoka kwa shairi guni. Ufuatao ni mpangilio wa mizani katika ubeti huo:

Mshororo wa Kwanza – Mizani (8,8)
Mshororo wa Pili – Mizani (7,9)
Mshororo wa Tatu – Mizani (10,8)
Mshororo wa Nne – Mizani (8,8)

6. Kikai

Kikai ni shairi lenye kipande kimoja kifupi (chenye mizani chache) kuliko kingine. Mfano (4,8) Neno ‘kikai’ linatokana na neno ‘kai’ lenye maana ya kusalimu amri au kuangukia mtu miguuni kama njia ya kukubali kushindwa. Katika historia ya ushairi mizani (8,8) kilikuwa ndicho kilele cha mshairi aliyefika kiwango cha umahiri. Basi aliyeshindwa kutunga shairi lenye mizani (8,8), alisalimu amri na kutumia mizani zilizopungua.

Mfano:

Natamani, lau tuu kukuona,
‘La mwendani, ni nafasi ndiyo sina,
Na lakini, tutakuja kukutana.
Ubaini, sisi si milima bwana,
Insani, sie hutembea sana,
Tu njiani, twatembea na twaona.
Rahmani,akipenda subhana,
Duniani, ijapokwamba ni pana,
Uamini, tutakuja kuonana.
Buriani, buriani wangu nana,
Salmini, wasalimu wangu wana,
Kwa yakini,tutakuja kuungana.

(Rashid Mwaguni)

Katika shairi hili, mtunzi ametumia bahari ya Kikai. Kipande cha kwanza kwa kila mshororo kina mizani 4 na cha pili mizani 8.

7. Upeo

Upeo ni shairi lililo na idadi tofauti ya mizani katika mishororo ya ubeti mmoja. Mshairi huipanga mishororo yake na kudhihirisha ujuzi wake. Tazama mfano wa shairi lifuatalo ‘Afrika Ina Homa’.

Mfano:

Afrika ina homa, inaumwa homa kali,
Taabani yatetema, zizimo la mwili,
Wenye macho hutazama, hii hali,
Na hawana la kusema, kweli,
Afrika ina homa!

Ina ndwele ya hujuma, hasama za majangili,
Na vikwazo vya kuchuma, vinavyotudhili,
Maradhi yanayochoma, bilikuli,
Dawa za usalama, ghali,
Afrika ina homa!

Huku roho zinauma, tepetevu maduhuli,
Viwanda bora vya chuma, bidhaa aali,
Vyauza kutoka nyuma, kule mbele,
Kunyonya wetu uzima, nduli,
Afrika ina homa!

(Wallah Bin Wallah E.A.E.P, Malenga wa Ziwa Kuu, Uk 132)