Najifunza Kufinyanga

Si kila wakati utanunua vifaa unavyohitaji. Wakati mwingine utajifunza jinsi ya kuviunda mwenyewe. Najifunza Kufinyanga


Najifunza Kufinyanga

Udongo au mchanga, nende wapi kaupata,
Nendapo nikaukonga, nambie bila kusita,
Nende Pemba au Tanga, mfinyanzi nikakuta,
Udongo nautafuta, nijifunze kufinyanga.

Ajuaye anambiye, taaluma naitaka,
Kazi niishuhudiye, nikiunde cha kupika,
Anoneshe nianziye, niunde kikaundika,
Mfinyanzi namtaka, chungu nikajiundiye.

Vyangu vimeharibika, kudumu vimeshadinda,
Ugumu umevitoka, viundwavyo vimekonda,
Kununua nimechoka, vya sokoni sivipendi,
Chungu changu nitaunda, chema kisichovunjika.

Sina mwema wa kusifu, aleunda kiwe heri,
Wateja nawaarifu, hawakipati kizuri,
Imeshakuwa ni hofu, kununua chungu shari,
Wafinyanzi wajeuri, wanofinyanga hafifu.

Kufinyanga nitajuwa, wafinyanzi wafe njaa,
Siriyo nimegunduwa, mno wametuhadaa,
Watalamu nabekua, nepukane na balaa,
Wambiye sijapumbaa, taaluma nitajuwa.

Udongo nitachanganya, angaa niunde changu,
Vifaa nitakusanya, nisibaki bila chungu,
Utalamu nitafanya, aniongozapo Mungu,
Wafinyanzi nawakanya, walipate onyo langu.

Kwa wingi nitafinyanga, nikaviuze sokoni,
Hadharani nitapanga, niviuze mitaani,
Walonge wanaolonga, mabingwa waso kifani,
Ufinyanzi naulenga, wa kunipiku ni nani?

Maoni 1 kwa “Najifunza Kufinyanga”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*