Ubeti

Ubeti ni kifungu cha maneno katika shairi ambacho kimepangwa kwa mishororo kadhaa. Ni fungu la mistari lenye maana kamili. Ubeti unaweza kulinganishwa na aya katika maandiko ya kinathari.

Kwa mfano, shairi lifuatalo lina beti tatu.

Mawazo yananiwasha, ukweli nisielewe,
Yale unayonipasha, kwengine ukawa siwe,
Mawenge unaonesha, mwafulani usifiwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

Moto unaukokesha, patulivu pako wewe,
Unapenda kutonesha, kikajikita kiwewe,
Kigeugeu wazusha, yako tusiyatambuwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

Tumaini limekwisha, kuaminiwa si wewe,
Twajua wanaotosha, lijulikanalo liwe,
Yote unayotupasha, lazima yatatuliwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

© Kimani wa Mbogo