“Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.” Mungu Awapenda

Mungu Awapenda

Watoto wote wenzetu, sikiza shairi hili,
Yapate maneno yetu, mengi yalio ya kweli,
Mambo tuyafanye yetu, tena tukiyakubali,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Tuchezapo kwa furaha, Mola wetu tumsifu,
Tuimbapo kwa madaha, na moyoni bila hofu,
Wimbo uwe wa furaha, Mungu wetu kumsifu,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Tuwatii watu wote, na tuwe watoto wema,
Twendapo pahali pote, sote tuwe na heshima,
Tusemapo mambo yote, yawe mema tukisema,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Tusiache kuwa wema, na watoto watiifu,
Tuvipende vitu vyema, na mambo mema tusifu,
Ya muhimu ni hekima, tena tuwe watiifu,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Jumapili ifikapo, sote twende kanisani,
Kanisani tufikapo, tusifu na tuombeni,
Adhuhuri ifikapo, turudi kwetu nyumbani,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Tukikanywa tusikie, tufuate ya wazazi,
Mengi tujifahamie, tunapoifanya kazi,
Ubongoni yaingie, tuyajue kwa uwazi,
Njooni nyote watoto, Mungu wetu awapenda.

Maoni 5 ya “Mungu Awapenda”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*