Kuboronga Sarufi

Huu ni uhuru mtunzi anaotumia kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au mdundo wa ushairi.  Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “changu chambo ninakupa” badala ya “ninakupa chambo chambo”.  Tazama mfano ufatao. Mtunzi amesema’ “Lasifika lako jina” badala ya “Jina lako linasifika”. Tazama shairi lifuatalo

Lasifika lako jina, iweje unajikana,
Utunzi wako wafana, hakunaye wa kuguna,
Wenyewe tumeshaona, takuwaje sifa huna,
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

Ungali mti mpana, iweje u mche tena?
Matawi sufufu una, mizizi inapindana,
Majaniyo yaungana, iweje hatujaona?
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

Uchache kwako hakuna, iweje sasa watuna?
Sipendi ya kulumbana, naogopa kugombana,
Akubariki Rabana, takuwaje hujaona?
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

Wajua kupanga vina, iweje una ujana?
Tungo zako za maana, zadhihirisha ungana,
Mtumbati mwafanana, yawaje ugumu huna?
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

Lolote la kombo huna, iweje mche wanena?
Sifa zako zashikana, lasambaa lako jina,
Lenye chuku ndilo sina, takuwaje nikikana?
Marijani ndiwe mti, wengine tungali miche.

(Kimani wa Mbogo)