Maana ya Ushairi

Shairi ni utungo wenye muundo na lugha ya kisanii na inayofuata utaratibu wa vina na mizani, hisi au tukio juu ya maisha au jambo na hufuata utaratibu maalumu wa urari na muwala unaozingatia kanuni za utunzi.

Ushairi ni sanaa ya kutunga mashairi kwa madhumuni ya kutumbuiza au kuelimisha. Shairi lililotungwa lazima liwe na maudhui na dhamira kwa kusudi la kupasha ujumbe. Kama kazi nyingine za fasihi, mshairi hutumia tamathali za usemi na wahusika ila ana uhuru wa kutumia lugha ilmuradi azingatie kanuni za ushairi.

Mgogoro umekuwepo kati ya wanamapokeo na wanamabadiliko kuhusu maana ya shairi. Wanamapokeo (wanajadi) wakisisitiza kuwa vina na urari wa wa mizani ndio msingi wa Ushairi wa Kiswahili. Wanamabadiliko (wanamapinduzi), ambao ndio washairi wa kisasa, nao wakidhibitisha kuwa si lazima shairi liwe na vina na urari wa mizani ili liitwe shairi la Kiswahili.