Raia anapomchagua kiongozi wake, huwa na matumaini kuwa atamwelekeza kwa njia inayofaa. Iwapo atahujumu haki ya waliomchagua, raia huwa na ghadhabu. Hebu litazama shairi hili… Ahadi Zitimizeni


Ahadi Zitimizeni

Uchaguzi mlishinda, mkawa mwajiamini,
Ahadi mlivyopenda, zikatimizwe kazini,
Mlitaja mkiranda, tukaupata uneni,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Sheria mkiziunda, kwa wote ziwafaeni,
Msibaki tu mwawanda, nasi pasi na mapeni,
Mtwae kwenu mabunda, tukilia mashinani,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Kutenda mmeshadinda, tangu muwe ofisini,
Kazi yenu kutulinda, haki musiweke duni,
Msije mkatupinda, mkidhani hatufani,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Imeshapita kalenda, badiliko hatuoni,
Hatutaki njia panda, mtuache taabani,
Msitoneshe kidonda, kwa misingi yenye inda,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Zitafuteni ajenda, wazalendo kuauni,
Waishio kwa vibanda, wahisi wana thamani,
Isiwe mali mwaponda, muwapo serikalini,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Tumebaki kama kinda, aishivyo kiotani,
Taharuki imetanda, tusijue tulikoni,
Viongozi wa ukanda, ni kwenu twatumaini,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

Twataka kuona tunda, litokalo kwa madeni,
Tena akichoka punda, usimpige mpini,
Yawezekana kurunda, bila kuweza nchini,
Mlisema mtatenda, ahadi zitimizeni!

© Kimani wa Mbogo (09/03/2023)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*