Beti

Ubeti ni kifungu cha maneno katika shairi ambacho kimepangwa kwa mishororo kadhaa. Idadi ya mishororo kwa ubeti hutambulisha aina ya shairi. Kwa mfano, tathnia ni shairi lenye mishororo miwili kwa kila ubeti. Tathlitha lina  mishororo mitatu na tarbia lina mishororo minne kwa kila ubeti.

Beti Katika Shairi

Tazama mfano ufuatao.

KILA SIKU NA MAWAZO

Ningekuwa na uwezo, mambo mengi ningejuwa,
Singetaka maelezo, mengi mngeyatambuwa,
Yamezidi matatizo, kiu yangu kuelewa,
Kila siku na mawazo, kuwaza na kuwazuwa.

Umeshazidi mkazo, mambo ya kufikiriwa,
Ya kutunukiwa tuzo, hakuna sijayajuwa,
Wajuvi wana mabezo, kwa hekima isokuwa,
Kila siku na mawazo, kuwaza na kuwazuwa.

Sijalipata liwazo, kwa yote yanisumbuwa,
Limebaki la chukizo, kila kutwa linatuwa,
Nimelifanya tangazo, watu wote wakajuvva,
Kila siku na mawazo, kuwaza na kuwazuwa.

Sijaupata mwongozo, kwa kina kufafanuwa,
Limebaki hanikizo, moyo unanisumbuwa,
Ningepata pendekezo, mengi ningeelezewa,
Kila siku na mawazo, kuwaza na kuvvazuwa.

Sipati kielelezo, kwa mambo nisiyojuwa,
Sijalipata agizo, yategwayo kuteguwa,
Napata wazo kwa wazo, na kamwe sijang’amuvva,
Kila siku na mawazo, kuwaza na kuwazuwa.

Shairi hili lina beti tano. Kila ubeti una mishororo minne. Vina vya kati ni -Zo na vya mwisho ni -Wa. Kila mshororo una vipande viwili na kila kipande kina mizani 8. Shairi lenyewe pia lina kibwagizo kwa jina “KILA SIKU NA MAWAZO”

Kichwa cha Shairi

Huu ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi moja. Anwani ni kidokezo muhimu kinachoelezea jambo linalozungumziwa katika shairi. Anwani huwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya kibwagizo. Shairi hupewa anwani inayoafikiana na maudhui au dhamira kwa  sentensi fupi.

Kutunga Ubeti

Tazama aya ifuatayo:
“Kilicho muhimu maishani ni heshima ili uweze kushinda na kuongoza. Cha muhimu ni hishima, ukitaka kuongoza. Hata ukiwa umeneemeka, si vyema kujipendekeza kwa mabaya. Ukiitaka huduma, haifai kila mtu ajue unalolitaka kwa kuwa ukikosa la kusema, ni vizuri kunyamaza.”

Kutoka kwa aya hii, mtunzi ametunga ubeti ufuatao.

Cha muhimu ni hishima, utakapo kuongoza,
Hata uwe na neema, baya kujipendekeza,
Uitakapo huduma, si vema kujitangaza,
Ukosapo la kusema, yakufaa kunyamaza.