Wanapochagulia hujitenga na waliowachagua kwa lengo la kujinufaisha. Ufadhili wao hutoweka na hisani kuadimika. Kura Yangu Huipati


Kura Yangu Huipati

Sifa zako ni kalili, ufadhili umesita,
Unao wingi wa mali, wakata wasiyopata,
Tumetambua ukweli, tumejua lilo tata,
Kura yangu ungepata, ungekuwa mfadhili!

Kivita twakukabili, mwafulani utajuta,
Tumechoka kwa kejeli, kwetu hizo zimekita,
Mheshimiwa hujali, kama unavyojiita,
Kura yangu ungepata, ungekuwa mfadhili!

Unajua yetu hali, Kwa matendo umesita,
Hayakufai makali, uanze zako kuteta,
Hutufaidi wakili, kwa mengi tunakusuta,
Kura yangu ungepata, ungekuwa mfadhili!

Muhimu ni maadili, maendeleo kuleta,
Yawache ya ubahili, walo wengi wanatweta,
Siasa kila mahali, masikio yakifata,
Kura yangu ungepata, ungekuwa mfadhili!

Yako hatutahimili, hatuyataki ya vita,
Ulianza kwa injili, wamaliza kwa matata,
Twaogopa ufidhuli, tena kwako kujibwata,
Kura yangu ungepata, ungekuwa mfadhili!

Maoni 6 ya “Kura Yangu Huipati”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*