Mshororo

Mshororo ni mstari mmoja wa maneno katika shairi. Idadi ya mishororo kwa kila ubeti wa shairi huainisha aina tofauti za mashairi.

  • Shairi la mshororo mmoja kwa kila ubeti huitwa tathmina.
  • Shairi la mishororo miwili kwa kila ubeti huitwa tathiniya, tathinia au uwili.
  • Shairi la mishororo mitatu kwa kila ubeti huitwa tathilitha
  • Shairi la mishororo minne kwa kila ubeti huitwa tarbia
  • Shairi la mishororo mitano kwa kila ubeti huitwa takhmisa
  • Shairi la mishororo sita kwa kila ubeti huitwa tasdisa au sudusia

Maelezo zaidi:

  • Mwanzo, Kifunguo au Fatahi mshororo wa kwanza katika ubeti
  • Mloto ni mshororo wa pili katika ubeti unaofuata mwanzo.
  • Mleo ni mshororo wa tatu katika ubeti unaofuata mloto
  • Kimalizio au Kiishio ni mshororo wa mwisho katika ubeti usiorudiwarudiwa katika kila ubeti.
  • Kibwagizo au Kiitikio ni mshororo wa mwisho katika ubeti unaorudiwarudiwa kila ubeti.

Ubeti ufuatao una mishororo mitatu.

Hata usake humwoni, hodari kwa yake kazi,
Hukusanya ya makani, yawe yake maongezi,
Udaku uso kifani, kwao wanayo ajizi.

Katika mfano unaofuata ni shairi la tarbia lenye mishororo minne kwa kila ubeti:

Si kwa maneno kulenga, ama nyingi atiati,
Haiwi hoja kupinga, urari kuwa bahati,
Hata vina kuvipanga, ingalipo mikakati,
Ushairi si kutunga, yapapo ya utafiti.

Ya shairi si kugunga, ya sheria hayasiti,
Kishairi ukilonga, sheria hadi tamati,
Yabidi ukajitenga, maktabani uketi,
Ushairi si kutunga, yapapo ya utafiti.

Funga safari ya anga, kwa lengo la kutafiti,
Upae wende Umanga, utayarishe ripoti,
Ufuate ya muwanga, kitumia yako hati,
Ushairi si kutunga, yapapo ya utafiti.

Usitunge na kuringa, limbukeni hujiiti,
Ukumbi unazo kunga, tena zilizo thabiti,
Msingi waliojenga, takuwa hadi tamati,
Ushairi si kutunga, yapapo ya utafiti.

© Kimani wa Mbogo