Shairi

Shairi ni utungo wenye muundo na lugha ya kisanii na unaofuata utaratibu wa vina na mizani, hisi au tukio juu ya maisha au jambo na hufuata utaratibu maalum wa urari na muwala unaozingatia kanuni za utunzi wa mashairi yanayohusika.

Mfano wa Shairi:

Shairi hung’aa, kwa ustadi utungapo,
Jema kuandaa, ushairi mwema upo,
Watu huduwaa, jema uliandikapo.

Haki itetee, usalama uwe kwako,
Tamu liwekee, japo vina vema viko,
Sifa zingojee, kwa umaarufu wako.

Waja elimisha, kupitia kwa shairi,
Bila kuwatisha, waelimishe ni heri,
Koja kukuvisha, halitakuwa la siri.

Mabaya waonye, bongo zao zionyeke,
Waja uwakanye, mema peke yatendeke,
Beti zikusanye, za maonyo uandike.

Watu waarifu, kupitia kwa ubeti,
Wa kusifu sifu, uandikapo kwa hati,
Watoe upofu, itakuwa ni bahati.

Watu changamsha, wadhiha waweze cheka,
Mema ukipasha, lazima kuchangamka,
Ubeti watosha, wacheke wakianguka.

Tunga kwa heshima, pasi matusi kufoka,
Taadhima sema, usemi mwema andika,
Usiseme lawama, mwanadamu kuteseka.

Oneka liweze, dhahiri lidhihirishe,
Lako litangaze, waziwazi lionyeshe,
Usilipoteze, hadharani ulipashe.

© Kimani wa Mbogo