Ujumbe

Ujumbe ni yale mambo ambayo mshairi angependa hadhira ijifunze ili kuweza kufanikisha misimamo iliyojengwa na msanii huyo. Kwa mfano, kama shairi linahusu bidii, ujumbe unaweza kuwa “Uvivu haufai na usipotia bidii maishani utaumia.”

Maudhui

Huu ni ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani. Maudhui hutumiwa kujenga dhamira ya shairi. Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi kutokana na kisa kilichomo katika shairi. Shairi linaweza kuwa na maudhui ya siasa, uchumi, mahaba, nk.

Dhamira

Hii ni mada, lengo kuu, wazo kuu, kusudi, madhumuni au nia ya mtunzi aliyokuwa nayo anapolitunga shairi lake. Alipotunga, alidhamiria kufanya nini? Mshairi hutunga shairi lake kwa lengo la kuelimisha, kuonya, kutahadharisha, kuliwaza, kuburudisha, kuhamasisha jamii, kukuza sanaa na ukwasi wa lugha, kuelekeza, kupitisha ujumbe, kusifia mtu/kitu, kukejeli au kukemea.  Baada ya kusoma shairi, unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli ipi.  Dhamira hutokana na mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.

Ujumbe wa Shairi

Unapolitunga shairi, ni lazima ujumbe wako ueleweke vilivyo. Ni vyema kila hoja ijitokeze kwa ubeti wake lakini hoja hizo ziwiane kwa kuunda dhamira ya shairi lako. Unapolitunga shairi, jiulize kama linastahiki kuelekezwa kwa hadhira ili kupasha ujumbe wako.