Tunapoelekea kwenye uchaguzi (Kenya), ni tumaini la kila mmoja kuwa hali ya utulivu na amani itakuwa. Wanasiasa wanaoshindwa watakubali na kuendelea na shughuli zao za maisha. Ukishindwa Ukubali


Ukishindwa Ukubali

Yanakera ya awali, yalokuwa hangaiko, 
Yabidi tukaamali, halifai tawanyiko, 
Haufai ujahili, utaleta mabomoko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Ateswaye ni madhili, kikamkumba kimako, 
Waonekao halili, huwa nalo badiliko, 
Huchafuka maadili, lingakosa kubaliko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Huyataka maduhuli, ila kwa misukosuko, 
Masuala hukabili, ukazua fadhaiko, 
Vema tukataamali, tulete mabadiliko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Twataka kura halali, lisije la taabiko, 
Unao wingi wa mali, kushindwa una vituko, 
Wazidisha ufidhuli, kwetu yawa hamaniko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Unapenda kukejeli, kila jambo una lako, 
Hishima zako kalili, kuonesha aibiko, 
Ya wengine hutajali, kwa hayo yako matuko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Unapokosa kibali, wacha yako ya zindiko, 
Ikubali yako hali, usilete ya tambiko, 
Amani kila mahali, pasiwe na la mauko, 
Ukishindwa ukubali, tuzuie machafuko. 

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*