“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yesu Ndiye Njia

Yesu Ndiye Njia

Tunaye alitufia, wingi wa zake neema,
Hasiti kutupatia, tunapohitaji mema,
Kwa baraka hututia, yatosha yake huruma,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Magumu yakiwadia, hutusimamisha wima,
Yesu ukimwitikia, baya halitakwandama,
Mazuri hukutakia, ukabaki u mzima,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Jua mnakoingia, muyatende ya heshima,
Muyawache ya dunia, mjue yana hatima,
Watu mkiwasifia, mnajitia lawama,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Tumwombalo husikia, tukimwita kwa hekima,
Baraka hutujalia, akatupatia hima,
Kwa Yesu tunapolia, hutufariji daima,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Kazi tukimfanyia, tusifanye twalalama,
Matendo hufurahia, iwapo yake huduma,
Sifa tunapomwimbia, kubariki hatakoma,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Tuwapo na njema nia, tutaipata rehema,
Ufanisi huwadia, kwa Yesu tukiinama,
Huwa tusiyodhania, Mungu huwa na huruma,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Lote ukitarajia, yabidi ukalisema,
Kwa Yesu litatimia, mwishowe uwe salama,
Jambo hulikubalia, liwapo la taadhima,
Yesu Kristo ndiye njia, ukweli hata uzima.

Maoni 2 ya “Yesu Ndiye Njia”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*