Zifuatazo ni Amri Kumi za Mungu:

1. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
2. Usijifanyie sanamu ya kuchonga.
3. Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako.
4. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.
5. Waheshimu baba yako na mama yako.
6. Usiue.
7. Usizini
8. Usiibe.
9. Usimshuhudie jirani yako uongo.
10. Usitamani…cho chote alicho nacho jirani yako.

Lisome shairi hili ambalo limetokana na hizi Amri Kumi za Mungu. Amri Kumi Za Mungu


Amri Kumi Za Mungu

Jua Mungu ndiye Bwana, Misri alikutoa,
Msujudu kwa mapana, Mungu anayekomboa,
Watumwa aliwaona, utumwa kawaondoa,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Usiifanye sanamu, vitu vilivyo mbinguni,
Usivichonge za humu, zilizomo duniani,
Mungu amezishutumu, kuzichonga za majini,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Bure usitaje jina, la Mungu alekuumba,
Jua huyo ndiye Bwana, sifa zake zimetamba,
La mzaha ndilo hana, umsifu na kuomba,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Ya Sabato ikumbuke, uitakase kwa mema,
Kazi nayo ifanyike, siku sita za huduma,
Ataka ieleweke, siku ya saba kukoma,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Heshimu baba na mama, siku utaongezewa,
Yatakikana heshima, siku umeahidiwa,
Utaipata neema, kwa mengi kubarikiwa,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Usiutoe uhai, mauaji ni hatia,
Twaambiwa haifai, kuwa nayo baya nia,
Maisha usiyadai, mwengine ukamwibia,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Imeelezwa kwa wazi, mwanadamu usizini,
Tiini ya mkombozi, msiwekwe taabani,
Wema nao hauozi, usiingie dhambini,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Usiibie mwenzako, Bibilia yakataza,
Ridhika na hicho chako, Mwokozi kukuongoza,
Kuiba kuna udhiko, kwa kweli kunachukiza,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Usitoe ya uongo, jirani kushuhudia,
Haifai kuwa mwongo, Bibilia yakwambia,
Unapofanya mipango, fanya ya kufurahia,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

Ya wengine usitake, vitu vyao kutamani,
Wanyama na vitu vyake, vya shambani na nyumbani,
Kiwache kilicho chake, tafuta chako makini,
Zielewe na kutii, amri kumi za Mungu.

KUTOKA 20:2, 4-17

© Kimani wa Mbogo (18/07/2013)

Maoni 1 kwa “Amri Kumi Za Mungu”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*