Awapo nazo tungo, mshairi hataikosa riziki. Wengi hudharau ushairi wakisema haulipi. Shairi hili linampa moyo mshairi chipukizi na kumwelezea kuhusu ushairi unaolipa. Mshairi Hafi Njaa

Mshairi Hafi Njaa

Utunzi wa Kimani wa Mbogo | Sauti ya Victor Mulama

Vina ameviandaa, maudhui na malengo,
Ujumbe unapong’aa, kwazo kuswifika tungo,
Zingapendwa zikafaa, cha ushairi kitengo,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Inapokuwa ridhaa, pasipokuwa simango,
Beti zake atazitwaa, zikaghaniwe ulingo,
Nyingine nazo idhaa, inapokuwa mipango,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Haimwangamizi baa, kikamwandama kifungo,
Wangamwona apumbaa, ana mengi kwa ubongo,
Ya hekima yamejaa, tamathali ni viungo,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Humpati asinyaa, ama aomba mchango,
Kumfanyia hadaa, huutambua urongo,
Hafuatwi na balaa, kikazuka cha kinyongo,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Yake hayajachakaa, ameyaremba mapingo,
Daima huwa shujaa, ana cha juu kiwango,
Hanalo la kushupaa, ama kuwa na maringo,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Swifa zake hutambaa, kama neno li kwa bango,
Washabiki huduwaa, thabiti kama mpingo,
Ana mengi kukomaa, akosapo liko pengo,
Mshairi hafi njaa, zingawapo zake tungo.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*