Wasemavyo “Elimu ni mambo yote” ni sahihi. Kila jambo linalofanyika duniani hutegemea elimu. Walioko shuleni watie bidii. maisha yao itategemea elimu waliyoipata shuleni. Ulishindwa ya Vitabu

Ulishindwa ya Vitabu

Imekuzonga aibu, ikadhihirika wazi,
Lilikuwa la ajabu, mitihani huiwezi,
Imekupata taabu, hujawa na la ujuzi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Huulizwi ukajibu, hunacho unamaizi,
Uliamua ububu, kukukera uchokozi,
Nilikupenda sahibu, ila unao ubozi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Kusoma ulijaribu, ukapata mapinduzi,
Hukuweza la kutibu, chuo kikawa makazi,
Walikubandika Babu, jina lako la majazi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Hukuwa nayo sababu, udhia hutuelezi,
Sipendi yalokusibu, kukuacha laazizi,
Kawatafute wahibu, waabuduo ajizi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Yakusubiri sulubu, wafanyavyo wajakazi,
Usingoje la dhahabu, hukuweza utambuzi,
Hungeweza utabibu, huhitaji uchambuzi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Ulibadili adabu, kujifanya mnyakuzi,
Umependa kughilibu, upate za maokozi,
Kila mtu mahabubu, utakalo humwelezi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Itakupata adhabu, likutiririke chozi,
Jina uliliharibu, ukaswifika u jizi,
Una wako uraibu, ulifanya uamuzi,
Ulishindwa ya vitabu, utawezaje ya kazi?

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*