Mwanakupona

1.
Negema wangu binti
Mchachefu wa sanati
Upulike wasiati
Asa ukazingatia

2.
Maradhi yamenishika,
Hatta yametimu mwaka
Sikupata kutamka
Neno lema kukwambia

3.
Ndoo mbee ujilisi
Na wino na qaratasi
Moyoni nina hadithi
Nimependa kukwambia

4.
Ukisa kutaqarabu
Bismillahi kutubu
Umsalie Habibu
Na sahabaze pamoya

5.
Ukisa kulitangaza
Ina la Mola Muweza
Basi tuombe majaza
Mola tatuwafiqia

6.
Mwanaadamu si kitu
Na ulimwengu si wetu
Walau hakuna mtu
Ambao atasalia

7.
Mwanangu twaa waadhi
Pamoya na yangu radhi,
Mngu atakuhifadhi,
Akuepushe na baa

8.
Twaa nikupe hirizi
Uifungeto kwa uzi
Uipe na taazizi
Upate kuyangalia

9.
Nikutungie kindani
Cha lulu marijani
Nikuvike mke shani
Shingoni kikizagaa

10.
Penda nikupe kifungo
Kizuri kisicho ongo
Uvae katika shingo
Utaona manufaa

11.
Yangu utakaposhika
Mwanangu hutosumbuka
Duniani utavuka
Na akhira utakia

12.
La kwanda kamata dini
Faradhi usiikhini
Na sunna ikimkini
Ni wajibu kuitia

13.
Pili uwe na adabu
Na ulimi w athawabu
Uwe mtu mahabubu
Kula utakapoingia

14.
La tatu uwe sadiqi
Wambiwalo ulithiqi
Mtu asoshika haqi
Sandamane naye ndia

15.
Tena mwanangu idhili
Mbee za maqabaili
Uwaonapo mahali
Angusa kuwenukia

16.
Wangiapo wenukie
Na moyo ufurahie
Kisa uwapeke mbee
Watakapokwenda ndia

17.
Ifanye mteshiteshi
Kwa maneno yasoghashi
Wala sifanye ubishi
Watu wakakutukia

18.
Nena nao kwa mzaha
Yaweteao furaha
Iwapi ya ikraha
Kheri kuinyamalia

19.
Wala situkue dhana
Kwa mambo usoyaona
Na kwamba na kunong’ona
Tahadhari nakwambia

20.
Sitangane na watumwa
Ilia mwida wa khuduma
Watakuvutia tama
La buda nimekwambia

21.
Sandamane na wainga
Wasyua kuitunga
Ziumbe wasio tanga
Wala kuwaqurubia

22.
Mama pulika maneno
Kiumbe ni radhi tano
Ndipo apate usono
Wa akhera na dunia

23.
Nda Mngu na mtumewe
Baba na mama wayuwe
Na ya tano nda mumewe
Mno imekaririwa

24.
Naawe radhu mumeo
Siku zote mkaao
Siku mukhitariwao
Awe radhi mekuwea

25.
Na afapo wewe mbee
Radhi yake izengee
Wende uitukuzie
Ndipo upatapo ndia

26.
Siku ufufuliwao
Nadhari ni ya mumeo
Taulizwa atakao
Ndilo takalotendewa

27.
Kipenda wende peponi
Utakwenda dalhini
Kinena wende motoni
Huna bundi utatiwa

28.
Keti naye kwa adabu
Usimtie ghadhabu
Akinena simjibu
Itahidi kunyamaa

29.
Enda naye kwa imani
Atakalo simkhini
We naye sikindaneni
Ukindani huumia

30.
Kitoka agana naye
Kingie mkongowee
Kisa umtengezee
Mahala pa kupumua

31.
Kilala siikukuse
Mwegeme umpapase
Na upepo asikose
Mtu wa kumpepea

32.
Kivikia simwondoe
Wala sinene kwa yowe
Keti papo siinue
Chamka kakuzengea

33.
Chamka siimuhuli
Mwandikie maakuli
Na kumtunda muili
Kumsinga na kumwoa

34.
Mnyoe mpatilize
Sharafa umtengeze
Na udi umfukize
Bukuata wa ashia

35.
Mtunde kama kijana
Asiyojua kunena
Kitu changalie sana
Kitokacho na kungia

36.
Mpumbaze apumbae
Amriye sikatae
Maovu kieta yeye
Mngu atakulipia

37.
Mwanangu siwe mkoo
Tenda kama uonao
Kupea na kosha choo
Sidharau mara moya

38.
Na kowa na kuisinga
Na nyee zako kufunga
Na smini kutunga
Na firashani kutia

39.
Nawe ipambe libasi
Ukae kama arusi
Maguu tia kugesi
Na mikononi makoa

40.
Na kidani na kifungo
Sitoe katika shingo
Muili siwate mwingo
Kwa marashi na daiia

41.
Pete sikose zandani
Hina sikome nyaani
wanda sitoe matoni
Na nshini kuitia

42.
Nyumba yako i nadhifu
Mumeo umsharifu
Wakutanapo sufufu
Msifu ns kumiaya

43.
Muyuwe alipendalo
Nawe ufuate lilo
Yambo limtukialo
Siwe mwenye kumwetea

44.
Na ukitaka kutoka
Sharuti rukhusa taka
Wonapo meudhika
Rudi na kuikalia

45.
Fuata idhini yake
Awe radhi kwa yaqini
Wala sikae ndiani
Saa yane ikasia

46.
Wala sinene ndiani
Sifiinue shiraani
Mato angalia tini
Na uso utie haya

47.
Rejea upesi kwako
Ukae na mume wako
Utengeze matandiko
Mupate kuilalia

48.
Mume wako mtukuze
Sifa zake zieneze
Wala simsharutiye
Asichoweza kutoa

49.
Akupacho mpokee
Na moyo ufurahie
Asolitenda kwa yeye
Huna haja kumwambia

50.
Uonapo uso wake
Funua meno uteke
Akwambialo lishike
Ilia kuasi Jalia

51.
Mama sinue ulimi
Nioleza wako umi
Nalioa nyaka kumi
Tusitete siku moya

52.
Alinioa babako
Kwa furaha na ziteko
Tusondoleane mbeko
Siku zote twaiokaa

53.
Siku moya tusitete
Ovu langu asipate
Na lake nisilikute
Hatta akakhitariwa

54.
Yalipokuya faradhi
Kanikariria radhi
Kashukuru kafawidhi
Moyo wangu katoshea

55.
Tangu hapo hatta yeo
Siyanyamaa kilio
Nikumbukapo pumbao
Na wingi wa mazoea

56.
Watu wakipulikana
Milele hukumbukana
Ilia wenye kushindana
Daima huiyutia.

57.
Mausio ya mvuli
Allah Allah yaamili
Na nduguzo na ahali
Wapende nakuusia

58.
Uwaonapo swahibu
Ambao wakunaswibu
Wakwambiapo qaribu
Angusa kuqurubia

59.
Na wachandika chakula
Uchambiwa nawe nia wala
Siweke muhula
Nyumanyuma kurejea

60.
Wala sifanye kiburi
Nia hata ushakiri
Usiyakuta siqiri
Ukamba ni kondolewa

61
Watu wote waumini
Kwako na wawe wendani
Sipende masalatini
Washinde ukiwepua

62.
Sipende wenye jamali
Na utukufu wa mali
Fuqara ukamdhili
Cheo ukamvundia

63.
Akupendao mpende
Akuizao mwenende
Kwa zema mvundevunde
Laana akiridhia

64.
Na ayaapo muhitaji
Mama kwako simuhuji
Kwa uwezalo mbuji
Angusa kumtendea

65.
Mama haya yasikize
Tafadhali sinipuze
Utaona nafuuze
Za akhera na dunia

66.
Tamati maneno yangu
Kukuusia mwanangu
Sasa tamuomba Mngu
Anipokelee dua

67
Kwani yote ninenao
Mwanaadamu ni puo
Mola ndiye awezao
Kupoteza na kongoa

68
Nakuombawe Manani
Umtilie auni
Ninenayo ulimini
Na yote nisoyatoa

69
Yote nimezoyanena
Rabbi taqabali minna
Na yasalieo tena
Rabbi Mola nitendea

70
Niwekea wangu wana
Na umbu iangu mnuna
Yakue yao maina
Yanee majimbo pia

71
Rabbi waweke nduzangu
Na wana wa ndugu zangu
Wende na ulimwengu
Kwa jamala na sitawa

72
Na jamii islamu
Mola wangu warehemu
Matakwa yao yatimu
Na nyoyo kufurahia

73
Ya Allahu wangu wana
Nimekupa ni amana
Watunde Mola Rabana
Siwate kuwangalia

74
Nimekupa duniani
Watunde uwakhizini
Unipe kesho peponi
Mbee za Tumwa Nabia

75
Wangalie kwa huruma
Waongoze ndia njema
Uwepulie na tama
Za akhira na dunia

76
Kukuombawe sikome
Wala sifumbi ulimi
Ya Mufarrija ‘1Hammi
Nikomeshee ushia

77
Nisimeme muhitaji
Mjao nakutaraji
Ajili bi’lfaraji
Ya afua na afia

78
Nondolea ndwee mbovu
Yaloningia kwa nguvu
Dhambi zangu na maovu
Ya Rabbi nighufma

79
Kwetu yangawa mazito
Kwako wewe ni matoto
Nepulia uvukuto
Uepuke mara moya

80
Nakuombawe Latifa
Unondolee makhafa
Kwa yaumu ‘1Arafa
Na idi ya udhia

81
Kwa siku hizi tukufu
Za kuhiji na kutufu
Niafu Rabbi niafu
Unishushize afua

82
Ya Ailahu ya Ailahu
Ya Rabbahu ya Rabbahu
Ya Gjayata Raghbatahu
Niyika hukwamkuwa

83.
Nakuombawe Rabbana
Bi amaila ‘Ihusna
Tisia wa tisiina
Mia kungua moya

84.
Nipulishie walimu
Wakinena yafahamu
Dua hini Islamu
Akiomba hujibiwa

85.
Nami mjao dhaifu
Mwenye nyingi taklifu
Nakuomba takhfifu
Rabbi nitakhafifia

86.
Nakuomba taisiri
Mambo nisoyaqadiri
Unengeshe kulla kheri
Shari ukinepulia

87.
Ya Rabbi nitimiliza
Mambo nisiyoyaweza
Wala moyoni kuwaza
Kwamba yatasikitia

88.
Rabbi unifurahishe
Mambo mema unengeshe
Maovu uyagurishe
Tusikutane pamoya

89.
Uniweke duniani
Miongo ya wahusuni
Nifapo nende peponi
Makao ya hafidhiwa

90.
Tungiie utungo hunu
Kwa zehemu na zitumu
Kwa qadha yako Dayyanu
Na hukumuzo Jalia

91.
Tungilie nili saqimu
Moyo usina fahamu
Usomeni Islamu
Mukiogozana ndia

92.
Na sababu ya kutunga
Si shairi si malenga
Nina kijana muinga
Napenda kumuusia

93.
Napenda kumkabihi
Laala katanabahi
Kamfuata illahi
Pamwe na wake rijaa

94.
Somani nyue huramu
Maana muyafahamu
Musitukue laumu
Mbee za Mola Jalia

95.
Somani mite ya nganu
Mutii waume wenu
Musipatwe na zitunu
Za akhera na dunia

96.
Mwenye kutii mvuli
Ndake jaha na jamali
Kula endapo mahali
Hutangaa yake ndia

97.
Mwenye kutunga nudhumu
Ni gharibu mwenye hamu
Na ubora wa ithimu
Rabbi tamghufiria

98.
Ina lake mufahamu
Ni mtaraji Karimu
Mwana Kupona Mshamu
Pate alikozaliwa

99.
Tarikhiye kwa yaqini
Ni alifu wa miyateni
Khamsa na sabiini
Hizi zote hijiria

100.
Na baitize idadi
Ni miati maadudi
Na mbili za mazidadi
Ndizo zimezozidia

101.
Mola tatusahilia
Kwa Baraka za Nabia
Na masahaba pamoya
Dini waliotetea

102.
Nahimidia kisalia
Kwa tume wetu nabia
Ali zake na dhuria
Itwenee sote pia.”