Iweje huifahamu wala kuishabikia lugha ya taifa ulikozaliwa? Iweje ukiabudu lugha za kigeni bila kuithamini lugha yako ya msingi? Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze. Kitukuzwe Kiswahili


Kitukuzwe Kiswahili

Ya heri tuyatangaze, tuibadilishe hali,
Tusiyoweza tuweze, hii lugha tusifeli,
Fani zote ziangaze, watu wote wakubali,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Wanafunzi tuwakaze, wakujue Kiswahili,
Wasojua tukataze, wabaki wanaojali,
Wanaoweza tutuze, lugha isiwe dhalili,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Mabingwa wajitokeze, ya hujuma tukabili,
Ya lugha tusiyabeze, hii dhana tubadili,
Maana tuwaeleze, wajue lugha aali,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Athari tusiongeze, tudumishe ya fasili,
Yaliyo bora tuwaze, tukijenge Kiswahili,
Manukato tuyajaze, la duni liwe muhali,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Lugha yetu tueneze, tuitee vikali,
Kamba tusiilegeze, lugha ibaki kamili,
Kwetu lugha ipendeze, tuyajue ya asili,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Kufunza tusinyamaze, kukuza iwe kauli,
Weledi tusichukize, hakika tusiidhili,
Hii lugha tuandaze, itambe kila mahali,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.

Heri tuicheze zeze, kwa maneno ya methali,
Ya lugha tuyaongoze, tukiinena halali,
Wajuao tusikwaze, hao ndio mihimili,
Kitukuzwe Kiswahili, lugha yetu tuikuze.​

© Kimani wa Mbogo (09/02/2023)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*