Utohozi

Hii ni mbinu ya kuswahilisha maneno kwa kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.  Kwa mfano, mtunzi anaweza kutumia “maikrowevu” badala ya “microwave.” Katika mfano ufuatao mtunzi ametumia neno “Palupiti” ambalo ni utohozi kutoka kwa neno la Kiingereza “Pulpit”.

Natuone ndipo twambe, kusikia si kuona,
Hili si kuamba, ukweli nimeuona,
Nitunga niliimbe, asilani lisofana,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Kasisi anasikika, neno katupakulia,
Palupiti azunguka, itikadi kututia,
Kasula kajipachika, Masihi kuhimidia,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

“Nyie kweli mwatamani, wala hamuwezi pata,
Kuomba mnaombeni, jibu hamjalipata,
Hamuombi kwa makini, ndo mwakawia kupata,”
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Ibada kawa nadhifu, kwao walio makini,
Kwangu ilikuwa hofu, baina yao wendani,
Waumini wakisifu, wahibu hawabaini,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Siti amejikwatua, usoni amemeteka,
Ghulamu jicho angua, mara anapokumbuka,
Haya yote kugundua, nikawa nafedheheka,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Ishara kwa kusanjari, usoridhisha wakati,
Msukosuko tayari, nilekuwa katikati,
Visura na yao siri, ghulamu na wake siti,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Kwangu mie nikajuta, kati ya wenzi wendani,
Kikingio wakapata, kaumu kuwa makini,
Langu ni kujikunyata, kama niko mvuani,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

Kwanza sujudu Kahari, baadaye ni mengine,
Haya tena yasijiri, hayo tena tusione,
Ishara kwa kusanjari, ibadani na kwengine,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.

(Kimani wa Mbogo)