Uainishaji Kuzingatia Vina

1. Mtiririko

Mtiririko ni shairi ambalo vina vyake vya mwisho na vya kati havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho. Iwapo shairi lina vipande vitatu kwa kila mshororo na vina havibadiliki kwa kila kipande kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho, pia huitwa shairi la mtiririko. Katika baadhi ya mashairi ya mtiririko, vina vya kituo (mshororo wa mwisho kwa kila ubeti) huwa ni tofauti na vya mishororo mingine ya ubeti.

Mfano:

Nasimama mlimani, ya mgambo kuiliza,
Isikike hadi pwani, na barani kupitiza,
Ifike na mapangoni, majoka kuyatokeza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Kikukosa ni gizani, sioni nabahatiza,
Hujikwaa madoleni, damu ikatiririza,
Njiani vyema sioni, macho huwa makengeza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Wavyele wangu mwendani, Abi nimeshawajuza,
Wanakungoja nyumbani, mapokezi memaliza,
Mama Tina shasaini, barakaze tatujaza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Kilala huja ndotoni, asali kunilambiza,
Tamu tena ya segani, si ya chupa lochachiza,
Kinidondoka nguoni, taratibu hupanguza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Sauti yako laini, isiyo ya kukereza,
Kiningia sikioni, hishi hamu kusikiza,
Tadhani ninga mwituni, tenzi akijiimbiza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Kinita taitikeni, takoma kinikataza,
Takutunza kimakini, kwa huba nikikutuza,
Sitokutenda yakini, hisiazo kuumiza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

Najitoa kileleni, wazi wazi shatangaza,
Sina niloyaficheni, wala niloyabakiza,
Meyatema ya moyoni, mengi nachia muweza,
Abi wewe yangu mboni, kikukosa huwa giza.

(Boniface K Wafula)

Hili ni shairi la mtiririko. Vina vyote vya ukwapi na vya utao ni havibadiliki kutoka kwa ubeti mmoja hadi mwingine. Vina vya ukwapi ni –ni na vya utao ni –za.

2. Ukara

Ukara ni shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine hubadilika. Kwa mfano, vina vya utao vinaweza kufanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho lakini vina vya ukwapi vibadilike kutoka ubeti mmoja hadi mwingine. 

Mfano:

Kipusa una vituko, twaviola hadharani,
Vyanambukiza udhiko, nikaliweka tungoni,
Vimekupumbaza vyako, wakuu wakulaani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

Kitwani zavurungana, si zetu si za kigeni,
Nywele zaangukiana, kisogo na utosini,
Ukadhani unafana, wende zako kinarani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

Wajihi wajipodowa, podari imo usoni,
Sana umejikwatuwa, ukijeleza rohoni,
Dhahiri hujang’amuwa, umaridadi hunani,
Si chochote si lolote, urembo wako siwoni.

(Kimani wa Mbogo)

Katika shairi hili, mtunzi ametumia bahari ya ukara. Vina vyote ya utao ni -ni lakini vya ukwapi vimebadilika kwa kila ubeti.

3. Ukaraguni

Tofauti na ukara, vina vyote vya ukaraguni hubadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, viwe ni vya ukwapi au utao. Neno guni ni kuwa na dosari au ila. Basi ukaraguni ni shairi lililotungwa bila kufuata kanuni za ukara. Iwapo kituo (mshororo wa mwisho wa kila ubeti) kina kipande kimoja tu au vina vyake havibadiliki, bahari hii hubainishwa kwa kuzingatia mishororo iliyotangulia kituo hicho.

Mfano:

Mja wa mateso miye, sina hili sina lile,
Waziwazi niambiye, sinibeze maumbile,
Singoje muda wadiye, kheri niambiwe mbele,
Miye dua nipigiye, Mwenyezi Yehova Jile.

Kazi ndiyo nitapata, pahali penye hishima,
Ujira mwingi kupata, licha ya njema huduma,
Changu cha pesa kitita, haki nipatge mapema,
Endapo utanifuta, niache nende salama.

Beti tatu zimetosha, sina muda kupoteza,
Kalamu nimekomesha, sina ya kusisitiza,
Mwajiri hutganitisha, mabaya ukitangaza,
Nipe ya pesa bahasha, japo hakuna nyongeza.

(Kimani wa Mbogo)

Katika shairi hili, vina vya ukwapi na vya utao vimebadilika kwa kila ubeti. Ni shairi la ukaraguni.

4. Masivina/Mapingiti

Masivina ni shairi lenye mwiano wa mizani lakini halina urari wa vina katika beti. Vina hubadilika mshororo hadi mwingine.

Mfano:

Sikiliza mawaidha, ufuate maagizo,
Uwambiwalo litende, yasikufike majuto,
Usitende utakalo, lisilo la maadili,
Zingatia ushauri, ni muhimu maishani.

(Kimani wa Mbogo)

Ubeti huu umenukuliwa kutoka kwa shairi la masivina. Kila mshororo una mizani 16 lakini vina vya ukwapi na vya utao ni tofauti kwa kila mshororo.

5. Shairi Huru/Mavue

Hili ni shairi lisilobanwa na kanuni zozote za kijadi za utunzi. Ni shairi linalokiuka arudhi au kaida za utunzi wa mashairi. Si lazima shairi liwe na idadi maalum ya mizani katika kila mshororo au mpangilio maalum wa vina. Mshairi anaweza kutumia mbinu zozote za utunzi/uandishi hata kuchanganya bahari kwa shairi moja.

Mtunzi hutumia mbinu mbalimbali za utunzi wa mashairi ili kulitofautisha na kazi nyinginezo za nadhari. Mtunzi anaweza kufupisha maneno (inkisari), kurefusha maneno (mazida), kutumia maneno teule ya kishairi au kutumia mafumbo.

Mfano:

Ningekua kikongwe yapata,
Ningezaliwa enzi za Robert,
Ningekuwa naye wa kuteta,
Ningekuwa rafiki, wa Shaaban Robert.

Tuzungumze kutwa mashairi,
Tufumbue fumbo la Liongo,
Utenzi wa mtu jasiri,
Ningekuwa rafiki, wa Shaaban Robert.

Ningefaidi tele zake busara,
Huyu baba wa akina adili,
Mtu asiye hata masihara,
Ningekuwa rafiki, wa Shaaban Robert.

Tungefikiri ya kufikirika,
Kwa lugha mama Kiswahili,
Tungesadiki ya kusadikika
Ningekuwa rafiki, wa Shaaban Robert.

Najua ningefuga madevu,
Masiyo makubwa nayosikia,
Kichwa chenye utulivu,
Ningekuwa rafiki, wa Shaaban Robert.

(Onesmo Joel)