Mishororo

Mshororo ni mstari mmoja wa maneno katika shairi. Idadi ya mishororo kwa kila ubeti wa shairi huainisha aina tofauti za mashairi. Kwa mfano, Tathlitha ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti.

Mshororo Katika Ubeti

Tazama mfano ufuatao.

Shairi hung’aa, kwa ustadi utungapo,
Jema kuandaa, ushairi mwema upo,
Watu huduwaa, jema uliandikapo.

Ubeti huu ulionukuliwa kutoka kwa shairi la tathlitha una mishororo mitatu. Kila mshororo umegawanywa kwa vipande viwili. Kipande cha kwanza huitwa Ukwapi.

Kipande cha pili katika mshororo huitwa Utao. Iwapo mshororo una kipande cha tatu, huitwa Mwandamo na cha nne ni Ukingo.

Mshororo wa kwanza katika ubeti huitwa Mwanzo, Kifunguo au Fatahi. Mloto ni mshororo wa pili katika ubeti unaofuata mwanzo. Mleo ni mshororo wa tatu katika ubeti unaofuata mloto.

Iwapo shairi lina mshororo wa mwisho kwa kila ubeti unaorudiwarudiwa, huitwa Kibwagizo au Kiitikio. Iwapo mshororo huo haurudiwirudiwi, huitwa Kimalizio/Kiishio.

Kutunga Mshororo

Mtunzi huwa na uhuru wa kubadilisha sauti (tabdili), kupunguza idadi ya mizani (inkisari), kuzidisha mizani (mazida), kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.

Tazama sentensi ifuatayo iliyoandikwa kwa lugha ya nadhari.

FULANI ATAJIINUA ILI PALIPO NA WATU AJITOME

Sentensi hii haina muundo wowote wa kishairi. Iwapo mtunzi angeitumia sentensi hiyo kama mshororo, angekuwa ametumia mizani 21 kwa wakati mmoja, bila kugawa mshororo wake kwa vipande vyovyote. Aina hiyo ya mshororo huenda ikawa na ugumu wa kuimba au kughani shairi lenyewe.

Iwapo mtunzi ataitumia sentensi hiyo kuunda mshororo, lazima abadilishe mpangilio, apunguze mizani ama atumie uhuru wowote ule alio nao. Tazama mshororo ufuatao ulioundwa kutokana na sentensi hiyo.

Fulani ‘taiiinuwa, palo watu kujitoma

Neno ‘atajiinua’ amelifupisha kwa kutumia mbinu ya inkisari na kuwa ‘tajiinua. Tazama alama ya (‘) inayomaanisha kuna silabi isiyotajwa kwa neno hilo. Maneno ‘palipo na’ yamefanywa kuwa ‘palo’ kwa kutumia mbinu iyo hiyo ya inkisari.