Tabdili

Ni uhuru wa mwandishi kubadilisha sauti na neno ili kufananisha vina. Kwa mfano mtunzi anaweza kutumia neno “upudhi” badala ya “upuzi”. Tazama shairi lifuatalo:

Hujipamba cheo kadhi, kumbe hana yake kazi,
Amezidisha upudhi, kwa ubaya wa malezi,
Hujibadikia hadhi, ila hanao ujuzi,
Kwa matuko anaudhi, ajifanyavyo mwamuzi!

Litendwalo alijuwa, maneno kusemasema,
Hajui tumetambuwa, hupenda anavyovuma,
Tena atajiinuwa, palo watu kujitoma,
Kumbe kadharauliwa, mwamuzi mwenye adhama.

Vilivyo hujionesha, tungo zake atungavyo,
Yuyo huyo kapotosha, anavyohadhiri sivyo,
Minarani hujinyosha, kwa tabia zake ovyo,
Hakuna wa kumpisha, anavyotenda visivyo.

Hutangaza hatujui, mwamuzi mjua yote,
Madaha hayapungui, wandikalo alifute,
Ameshakuwa adui, marafiki asipate,
Mpate mwamuzi mui, ukiweza umfate.

Mwamuzi hujua mengi. ajuavyo ni mjuvi,
Maneno yake kwa wingi, mara alete ugomvi,
Mwamuzi yeye hatungi, uamuzi ndo ugavi,
Kinywache nacho hafungi, kelele kama mlevi.

(Kimani wa Mbogo)