Uainishaji Kuzingatia Dhamira

1. Zivindo

Huu ni mkondo wa shairi unaojengwa kwa maana mbalimbali za maneno kutolewa. Hupatikana sana kwa ushairi wa jadi. Hufafanua maana za maneno. Kazi yake ni kujifunza na kuhifadhi lugha.

Mfano:

Kisu kutumia, mamba kuparuza,
Usafi kutia, papa au pweza,
Muda kuwadia, samaki paruza,
Iyo hiyo ndiyo, maanake paa. 

Kwa sasa igiza, jifanye yu nyuni,
Mwenyewe onyeza, tuende angani,
Mbinguni angaza, huko mawinguni,
Iyo hiyo ndiyo, maanake paa. 

Makaa chukuwa, utoe mekoni,
Pweza atakuwa, uwe hatarini,
Kaa hupaliwa, kuwa tazizoni,
Iyo hiyo ndiyo, maanake paa.

Mnyama porini, mbuzi usimwite,
Pembe za kichwani, huyo umpate,
Umwone mwituni, yule asisite,
Iyo hiyo ndiyo, maanake paa.

Jenga nyumba ewe, juu tafunika,
Bati, kuti, jiwe, moja utaweka,
Nyumba njema iwe, iliyonjengeka,
Iyo hiyo ndiyo, maanake paa.

 (Kimani wa Mbogo)

2. Malumbano

Huu ni utunzi wa mashairi ambapo mshairi mmoja hutunga shairi akijibu au kupinga utunzi wa mshairi mwenzake aliyetangulia kutunga. Wanaohusika hufumbiana, husemana, hugombana au huonyesha ufundi kwa kujinaki na kujifaragua. Mara nyingi anayejibu hutunga hutumia aina moja ya shairi kama la aliyetangulia; mishororo, mizani na vina.

Mfano:

Kimani wa Mbogo:

Tungabaki kubishana, mpwani ataumia,
Hatasema la maana, aambe tukasikia,
Hajaona la kufana, debe pwani apigia,
Mpwani yu Nairobi, pwani hakunazo kazi? 

Mpwani pwani ahama, akaja kuishi bara,
Kwa kweli bara ni kwema, kuutafuta ujira,
Maisha pwani si mema, hakunazo kazi,
Mpwani yu Nairobi, pwani hakunazo kazi? 

Mkimbizi hujigamba, hajibaini aliko,
Vita kuu vingabamba, hubaki na taabiko,
Maumivu humkumba, akawa nacho kimako,
Mpwani yu Nairobi, pwani hakunazo kazi?

Swila Mchiriza Sumu:

Kazi ni nyingi sana, tena nzuri za kufaa,
Wametuita mabwana, wenye kazi na vifaa,
Mana ujuzi hamna, kazi yenu ni kukaa,
Tunafanya Nairobi, Tunawekeza Mombasa!

Hauna wa kubishana, katika hiki kifaa,
Kiwango chako kijana, ni bado unatambaa,
Hujaweza kupigana, ili uitwe shujaa,
Tunafanya Nairobi, Tunawekeza Mombasa!

Vile ninavyokuona, hoja zimekuambaa,
Sasa unadanadana, ukitafuta shufaa,
Umeshawekwa kwa kona, kila kitu ni balaa,
Tunafanya Nairobi, Tunawekeza Mombasa!

Katika mfano huu, mshairi wa kwanza kupitia kwa shairi lake anauliza kwani pwani hakuna kazi kwa kuwa wapwani wanafanya kazi mjini Nairobi. Mshairi wa pili naye anamjibu kuwa Wapwani hufanya kazi jijini Nairobi lakini pwani ndiko wanakowekeza. 

3. Taabili

Taabili ni shairi ambalo hutungwa kwa nia ya kumsifia mtu aliyeaga dunia.

Mfano:   

Humu tu wapita njia, kesho haijulikani,
Majonzi limetutia, likatanda la huzuni,
La mno limetukia, katukumba ukumbini,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Imetuchukua muda, jambo hili kukubali,
Tumefikwa nayo shida, wapenzi wa Kiswahili,
Twakumbuka zako mada, lugha ulivyoijali,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Pakubwa ulichangia, bidii zako mwalimu,
Pengo umetuwachia, pote ulipohudumu,
Kwa mengi umepitia, ughaibuni na humu,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

(Kimani wa Mbogo)