Mwanafunzi hapa anasifia hali yake ya mazoea. Kuamka na kuelekea shuleni kwa sababu moja tu; kutafuta elimu. Lisome shairi hili: Elimu Nimeipata


Elimu Nimeipata

Mapema niamkapo, haraka hujiandaa,
Hamamuni niogapo, sare zangu kuzivaa,
Mkoba nichukuapo, huwa nimejiandaa,
Tangu shule nijiunge, elimu nimeipata.

Hungoja gari la shule, asubuhi na mapema,
Shule nifike mbele, saa moja kusimama,
Nisome liwalo liwe, niwe mwema nikisoma,
Tangu shule nijiunge, elimu nimeipata.

Kiswahili kingereza, sayansi nahisabati,
Ubongoni huongeza, nikiketi kwa dawati,
Yeyote hunipongeza, vema kuandika hati,
Tangu shule nijiunge, elimu nimeipata.

Wazazi wetu sikiza, mtie hili vichwani,
Lugha yangu kingereza, hiyo niongelesheni,
Umombo nimaujaza, ukajazika kichwani,
Tangu shule nijiunge, elimu nimeipata.

Beti tano zimefika, shairi natamatisha,
Mungu naomba baraka, shule yetu neemesha,
Nambari moja kushika, wengine tukikomesha,
Tangu shule nijiunge, elimu nimeipata.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2006)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*