Hata waseme nini, umpendaye unampenda. Hili ni shairi la mahaba. Mtunzi anamsifu mpenzi wake kwa maneno anayodai yanatoka moyoni mwake. Lisome shairi lenyewe. Ninakupenda Mpenzi Wangu


Ninakupenda Mpenzi Wangu

Kwangu ninayo faraja, moyo sina hatihati,
Wewe ni nambari moja, mwengine mie sioti,
Nikuvike lipi koja, nikupendaye kwa dhati,
Ninakupa hii hoja, ya kukusifu siati.

Kwa kaumu nahadhiri, pendo langu sikuhini,
Mie nina ikirari, yako yamo mawazoni,
Ninakupa yangu siri, niliyo nayo moyoni,
Yako nikitafakari, hayanitoki kichwani.

Hata wakuite jizi, daima wewe ni wangu,
Pachipachi yao wezi, pendo ninakupa langu,
Sendi omo wala tezi, siutaki wingi kwangu,
Siwastahi wagwizi, kwako kukufunga pingu.

Wewe ninayekupenda, mpenzi ulozaliwa,
Hujua unavyolinda, neena ulijaliwa,
Mpenzi wangu washinda, pa mshindi umwetiwa,
La upendo sitadinda, kwa wingi nitalitowa.

Mengi mie sisaili, naujua wako wema,
Pendo lako si la mali, ni kwa mabaya na mema,
Sikufiti langu hili, nilojua tangu zama,
Upendwaye tasihili, huna neno la lawama.

La kukuficha sinalo, sikuchezei kindani,
Pendo langu nikupalo, latoka kwangu moyoni,
Lolote litendekalo, jua wewe u mwandani,
Nataka welewe hilo, tena uwe na imani.

© Kimani wa Mbogo (01/07/2006)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*