Aitwaye mwananchi wa kawaida ana haki zake? Na kama anazo, anazielewa kweli? Lisome hili shairi… Zipi Haki Zangu?


Zipi Haki Zangu?

Nyote mawakili,zipi haki zangu?
Enyi jibu hili, nizijue zangu,
Wabunge ukweli, zipi haki zangu?
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Wote nauliza, kisha wanijibu,
Ninaona kiza, sipati jawabu,
Sauti napaza, nilipate jibu,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Haki nazitaka, haki za yatima,
Nimetaabika, sina yangu mema,
Nimedhoofika, mie nimezama,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Kushoto maafa, sizipati haki,
Kulia maafa, sizioni haki,
Mbela nyuma afa, hakutemeleki,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Nendapo nyumbani, ninahujumiwa,
Nendapo shambani, ninashutumiwa,
Nendapo shuleni, ninahasimiwa,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Daima nalia, kilio daima,
Daima kulia, lini nitakoma,
Kwenu nitalia, babangu na mama,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

Kuhoji sikomi, zipi haki zangu?
Yatima sikomi, nizijie zangu,
Haki nijihami, nikipata zangu,
Nauliza swali, zipi haki zangu?

© Kimani wa Mbogo (01/01/2006)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*