Ya kesho ni ya Mungu. Hujui wakati na wasaa wa kifo chako. Hivyo basi tegemea Mungu muumba wako kwa vyovyote vile. Anao uwezo wa kukulinda na kukuweka hai. Leo tu nina uhai


Leo tu nina uhai

Unaniona ni’ hai, niishivyo duniani,
Siuoni ulaghai, kwa waloenda kifoni,
Walonena leo hai, kesho kuwafuateni,
Leo tu nina uhai, kesho haijulikani.

Afadhali hayawani, aliye nao uhai,
Daima yeye haneni, akisema hayafai,
Keshoye kichinjioni, maisha hatayadai,
Hili kwangu li wazoni, nitapoteza uhai.

Maisha ni kama ua, asubuhi huchanuka,
Jua utosi kutua, ua nalo laanguka,
Uhai ni kama ua, kesho kifo chanidaka,
Leo tu napokechua, kesho kaburi mwaaka.

Kuzimu ninakuenda, pindi kifo kunigwia,
Huzuni kwenu yatanda, huko ninapoingia,
Usidhani sitaenda, ahera ikinibwia,
Masikitika kutanda, kaburini kunitia.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*