Anapozuru nchini watu humsifu na kumumiminia swifa tele. Wasije kumwabudu kama ndiye mungu wao. furahia uhondo wa shairi hili… Kuzuru Kenya si Hoja

Kuzuru Kenya si Hoja

Si la chuki ninataja, kishairi kuliamba,
Nanena palipo haja, kwa maoni nikalumba,
Mnavyokosa faraja, adinasi kumuimba,
Kuzuru Kenya si hoja, mwanadamu si Muumba!

Kiongozi ni mmoja, sifa Kenya zikatamba,
Mwamvalisha kingaja, kumtukuza wa chemba,
Mwengine mwampembeja, kwa sifa mkimpamba,
Kuzuru Kenya si hoja, mwanadamu si Muumba!

Hupekua ya kufuja, kwa kina akituchimba,
Kwa sasa mwampa koja, kwa maneno ya kuremba,
Kwao huwa na daraja, wanakojua yu mwamba,
Kuzuru Kenya si hoja, mwanadamu si Muumba!

Wengi wa heshima huja, wasio wa kujigamba,
Wameshakuwapo waja, thabiti wasioyumba,
Hayapo aliyongoja, heri tuwe ombaomba,
Kuzuru Kenya si hoja, mwanadamu si Muumba!

Tunaposubiri tija, twazidi kukaza kamba,
Hata akenda unguja, macho yetu tutafumba,
Hatutaki ya viroja, yajayo ya kutukumba,
Kuzuru Kenya si hoja, mwanadamu si Muumba!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*