Jambo moja la msingi taifa kuendelea ni Amani. Wanasiasa watakuwa na maoni mbadala, ila hilo ndilo jambo la muhimu. Lisome hili shairi uelewe zaidi. La Muhimu ni Amani


La Muhimu ni Amani

Inatupasa kupanga, kila jambo kwa makini,
Tujue tunayolonga, kwa kila wetu uneni,
Tuwapo na la kulenga, twafaulu hatimani,
La msingi ni amani, kwa taifa kulijenga.

Tukomeshe la kupinga, litwajwalo sheriani,
Zetu tungapozitunga, twajipata kizimbani,
Maovu tukijitenga, taifa twalitamani,
La msingi ni amani, kwa taifa kulijenga.

Vita silo la muwanga, suluhu hionekani,
Hawakosi wa kukonga, waupendao uhuni,
Wakale tukiwalunga,  tutapenda za usoni,
La msingi ni amani, kwa taifa kulijenga.

Kwa wazee na wachanga, tufuate ya zamani,
Ni vema tukijikinga, tuhimili za tufani,
Kibwewe tukijifunga, tutafaulu mwishoni,
La msingi ni amani, kwa taifa kulijenga.

Tunafozificha kunga, zisipatwe ugenini,
Tufanyayo tukichunga, tutakuwa tu wandani,
Haiwi kulengalenga, tuwapo nayo imani,
La msingi ni amani, kwa taifa kulijenga.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*