Sijui kama unamfahamu vema jirani yako au mtu mnayeshirikiana naye kwa karibu mno. Na suala la “Nyumba Kumi”  linapotajwa sijui linaibua hisia gani kwenye fikra zako. Baadhi ya watu tunaoishi pamoja, huenda wasikufae kwa chochote au lolote.

Wengine watakutumia, wakunongeshe na kukudhalilisha, hasara kwako. Wengine ni wanafiki wasio na utu, wasiokutendea lolote la hisani. Hata kama utamwamini aliye karibu nawe, usimtegemee wala ukadhani ni malaika kwako. Hili halimaanishi wewe usimtendee wema. Tenda wema nenda zako.

Shairi lifuatalo linaelezea kwa kina suala hili. Mhusika anahofia kwamba mtoto wake ataumwa na jibwa la jirani. Hili lalinganishwa na maovu anayoweza kufanyiwa na jirani yake. Ni shairi linaloonya kuhusu ushirikiano wako na jirani au mwandani wako wa karibu. Linamfahamisha hatari zinazomkabili kuwa na jirani asiye na matendo mema. Jibwa Litaniumia Toto


Jibwa Litaniumia Toto

Ninautoa uneni, nieleze kwa uketo,
Niitangaze ilani, limenijia fukuto,
Nitafute wa kughani, mlidake kwa fumbato,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Naeleza hadharani, sielezi kwa mkato,
Hili jambo halifani, natangaza wangu mwito,
Hakuna raha nyumbani, imezidi rangaito,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Natishwa na hayawani, apendwaye kama vito,
Nakosa la kuamini, hali hii ya mpwito,
Nimewaza kwa makini, usinipate mvuto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Litajificha uani, kulia ama kushoto,
Lishambulie mgeni, na yeyote kwa mseto,
Ukilipata pembeni, hukosi kuona moto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Hutalikosa langoni, linao upana mato,
Halinalo la utani, linaisaka mipito,
Heri niwe silioni, nayahofia majuto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Sinayo mengi mapeni, akatibiwe mtoto,
Fimbo tawa mkononi, bakora ama ufito,
Nikiviwacha chumbani, jibwa taligonga ngoto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Mwanangu namthamini, ni kama langu liwato,
Nitamlinda yakini, asitumie magwato,
Asijipate shakani, limzidie kunyato,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*