Kiongozi wa watu anapoondoka, huwa ni majonzi tele kwa wananchi , jamhuri na dunia yote kwa jumla. Halo ndivyo ilivyo tunapoomboleza kifo cha raisi wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mungu ailaze roho yake Rais John Pombe Magufuli mahali pema peponi. Kwaheri Magufuli


Kwaheri Magufuli

Hatunalo la kusema, ila sasa kukuaga,
Kifo hakina huruma, wakubwa huwatitiga,
Hata wale huwa wima, hakikosi kuwabwaga,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Kusema tumeshachoka, kauli katuishia,
Hima hima umevuka, huzuni ikatukia,
Majonzi yamewafika, hino nyota kufifia,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Maendeleo si haba, kwa hayo walikupenda,
Tena ukawa u baba, kwa wakata ulitenda,
Ulipotoa hotuba, kwa maneno hukudinda,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Umati ulifurika, uwapo kuhudhuria,
Huruma ilikufika, shida kuwatatulia,
Kote ulitambulika, mengi ulowafanyia,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Wengi walikutambua, mkakamavu jasiri,
Ya kwako tukagundua, kuyabaini dhahiri,
Mengi uliyajua, ukawa na umahiri,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Safiri nenda salama, dunia njia ni moja,
Hata uwapo kavuma, siku yako moja yaja,
Lazima kitakwandama, uwapo kifo kikaja,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Mapenzi huwa kwa Mungu, mwa’damu hana hanani,
Kwetu hubaki uchungu, kilio kikasheheni,
Litandapo hilo wingu, hukuishia utani,
Buriani Magufuli, Mola akulaze pema.

Maoni 4 ya “Kwaheri Magufuli”

  1. Mungu mwema Kwa shairi lenye simanzi na majonzi linalowakumbusha watu kuwa kifo kipo TU hata iwaje hivo upende usipende iwapo zamu Yako itafika basiiii utasimama kwenye zamu Yako, kwenye maisha Kuna mambo ambayo mtu unaweza kutaka mtu asimamie Kwa ajili Yako lakini sio swala la kifo kitakapo kuita basi utaitika,na kitakapo kufuata basii utaongozana nacho!!!! Hivyo tusisababishe vifo Kwa wezetu Bali Kila mumoja Kwa nafasi yake asubili zamu yake ahsante mtunzi kuelimsha nchi yetu Tanzania. MUNGU bariki viongozii wa nchii na uwashike mkono na uwaongoze….

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*