Siha ni majaliwa. Uwapo mzima, shukuru Mungu. Yapo maradhi yasiyomsikia mgonjwa wa mganga. Tazama shairi hili… Hunalo la Afueni


Hunalo la Afueni

La wazi nimetambuwa, hakika nikabaini,
Dhahiri nimeelewa, likanijaa wazoni,
Lilo muhimu si dawa, amani kuwa moyoni,
Licha yako kutibiwa, hunalo la afueni!

Mafumbo tumetatuwa, mengi tuliyoyadhani,
Mashakani umetiwa, ni ugonjwa si utani,
Mbio umetimuliwa, ukaisha ukingoni,
Licha yako kutibiwa, hunalo la afueni!

Kiwewe umeingiwa, kudhoofika mwilini,
La fahamu kupotewa, udhaifu ubongoni,
Waganga wa kuswifiwa, hawanalo kubaini,
Licha yako kutibiwa, hunalo la afueni!

Kwa muda umeuguwa, tena ikawa huponi,
Maradhi kujitanuwa, vema yakakubaini,
Haya yamekubambuwa, ukawa huna hunani,
Licha yako kutibiwa, hunalo la afueni!

Wauguzi kapagawa, hawanalo la makini,
Kuganga na kuganguwa, limekwama maishani,
Ni mengi yameshakuwa, si machache ulodhani,
Licha yako kutibiwa, hunalo la afueni!

Maoni 2 ya “Hunalo la Afueni”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*